• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
CORONA: Mshubiri kwa hoteli za kifahari

CORONA: Mshubiri kwa hoteli za kifahari

MARGARET MAINA NA RICHARD MAOSI

Tangu Waziri wa Afya Mutahi Kagwe atangaze kisa cha kwanza cha Covid -19 nchini, kulizuka tumbojoto miongoni mwa wamiliki wa mikahawa na maduka ya kuuza bidhaa kwa bei ya kijumla.

Wauzaji wengi hatimaye walliamua kujaza akiba ya vyakula, maji na vyombo vya usalama kwa ajili ya ongezeko la mahitaji ya vifaa hivi kwa wanunuzi.

Hali ni kama hiyo katika mkahawa wa kifahari wa ALPS, eneo la Milimani Nakuru, ambapo Taifa Leo ilibaini ni marufuku kuchukua hela mkononi.

Wakati wa mahojiano haya sehemu ya kuegesha magari ilikuwa tupu, vyumba vya malazi havikuwa vimepata wageni katika mkahawa huo ambao una vyumba 35, na sehemu ya kuogelea pembeni.

Meneja mkuu John Kiruthi anasema mkahawa wa Alps unadumisha usafi wa hali ya juu, wafanyikazi wakishauriwa kusafisha kila mahali, ili kutoa hakikisho kwa wageni na wenyeji.

“Tumekadiria hasara kubwa ikizingatiwa tunamiliki matawi mawili ya wafanyikazi 180, wanaoshughulika Nakuru na KCB Leadership Centre Nairobi,”akasema.

Wakati wa mazungumzo haya Kiruthi anasema alikuwa amefutilia mbali safari ya watalii kutoka Ujerumani, ambao wangetoa milioni tano kugfharamia malazi na vyakula.Isitoshe idadi ya watalii wanaoingia Nakuru imepungua.

“Tumeweka mikakati kuhakikisha wafanyikazi wetu wanaendesha shughuli katika mazingira safi kwa kuwahimiza wavalie vifaa vya kuziba mapua na kupima viwango vya joto mwilini kila mara,”akasema.

Kiruthi anawashauri wamiliki wa mikahawa mingine kuwa tayari kukabiliana na mkurupuko wa Corona, ambao kufikia sasa ni visa nne vimeripotiwa na serikali.

“Vyakula vyetu huandaliwa vyema na kuhifadhiwa ndani ya majokofu, ili wanunuzi wasipate matatizo ya kiafya yanayoweza kutokana na chakula kibovu,”aliongezea.

Wauzaji wa chakula cha kuzungusha, baa na sehemu za burudani wakionekana kupata pigo zaidi, wengi wao wameona ni afadhali wabakie majumbani pao badala ya kutangamana kwenye kumbi za starehe.

Bi Josephine Obote wa Aramatose Restaurant amekuwa akifanya kazi ya kuzungusha chakula, ndani ya benki na ofisi lakini sasa anaona italazimika afunge kazi kwa sababu sehemu za kazi zimebakia kuwa mahame.

“Nimeajiri vijana watano na pia ninalipia umeme na kodi ya nyumba, aidha ninagharamika kununua vyombo vya kudumisha usafi kama sabuni ya Dettol na huenda hivi karibuni nitafunganya virago, hususan tangu serikali itoe agizo la wafanyikazi kuchapa kazi kutoka nyumbani,”akasema.

Hatua chache kutoka hapo, tunakumbana na Leonard Kamau anayefanya kazi katikati ya mji wa Nakuru. Leonard anamiliki mikahawa mitatu katika barabara ya Kenyatta, anasema amekadiria hasara kuanzia siku tatu zilizopita.

“Tunapoteza wateja kila siku, ikizingatiwa kuwa mimi huagiza vyombo vyangu kutoka China ili kuendesha shughuli ya kutengeneza juisi ya matunda na meko za kisasa kupikia chakula,kwa idadi kubwa ya wateja”akasema.

Aliongezea kuwa tangu weita waanze kuvalia glavu na vifaa vya kujifunika usoni, baadhi ya wateja walianza kujawa na wasiwasi wakatoweka na kukwamisha shughuli.

Wachuuzi wanaomiliki mikahawa midogo midogo wanalazimika kumwaga chakula kila siku, huku baadhi ya wateja wakiamua kula chakula kutoka makwao.

Wateja kadhaa waliokubali kuzungumza na Taifa Leo wanasema wanaogopa kushika sahani, vikombe au kutangamana na walaji wengine wakihofia kuambukizwa virusi vya Corona.

Wengine waliopata pigo ni wauzaji matunda na samaki. Kulingana nao wanasema wateja wamekataa kutembelea vibanda vyao kufuatia tishia la Covid -19.

Kwingineko George Kihara meneja katika klabu maarufu ya SEBS, Nakuru anasema, ameshangaa kuona jinsi mambo yamebadilika kwa haraka, wateja wamepungua kuhudhuria matamasha katika mkahawa wao.

“Tumeweka mikakati yote kuhakikisha wanunuzi wetu ni salama lakini bado hali ya biashara ni mbaya,na huenda ikachukua muda kabla ya hali ya kawaida kurejea,” aliongezea.

You can share this post!

Magugumaji na kemikali kero Ziwa Naivasha

Rush United inavyokuza soka Nakuru

adminleo