Isiolo Starlets walenga ubingwa fainali za Chapa Dimba
Na JOHN KIMWERE
TIMU ya wasichana ya Isiolo Starlets itakuwa miongoni mwa vikosi saba vitakavyoshiriki fainali za kitaifa kuwania taji la Chapa Dimba na Safaricom Season Three mwaka huu.
Kwa mara ya kwanza vigoli hao watakuwa wakiwakilisha Mkoa wa Mashariki baada ya kushinda kwenye fainali zilizopigiwa uwanjani Kenyatta Stadium, Machakos.
”Kusema kweli tunashukuru kwa kutimiza azma yetu kubeba ubingwa wa taji hilo na kujikatia tiketi ya kushiriki fainali za kitaifa,” alisema meneja wake, Aden Hussein na kuongeza kuwa wanapania kutifua vumbi kali kutafuta ubingwa wa kitaifa na kutuzwa kitita cha Sh1 milioni.
Alisema kuwa ufanisi haukuja kiulani mbali walijikakamua kadiri ya uwezo wao. ”Nina imani tosha wachezaji wangu siyo mende ambapo endapo wapinzani wetu wakiteleza tu tutapitia katikati yao na kutawazwa malkia wa kipute hicho.
Sina shaka kutaja kwamba kwenye fainali za Mkoa wapinzani wetu walitudharau lakini tulifanikiwa kuwabwaga na kujikatia tiketi ya kutufikisha katika fainali za kitaifa,” alisema.
Naye kocha wake, Hussein Wako alisema kuwa mlipuko wa virusi hatari vya korona umewanyima nafasi ya kuendelea na mazoezi yao lakini hawana budi ila watasubiri wakati wa Mungu hali itakaporejea kawaida.
Vipusa hao walishiriki fainali za Mkoa baada ya kushinda mechi mbili katika kiwango cha Kaunti ndogo ya Meru na Maua.
”Tulipitia pandashuka nyingi ili kutinga fainali za kitaifa hasa kushawishi wazazi kuruhusu wanao kushiriki mechi hizo,” alisema na kuongeza kuwa ulikuwa mwanzo wa ngoma wanatarajia mafanikio zaidi siku sijazo.
FAINALI
Isiolo Starlets chini ya kocha, Hussein Wako na Collins Otieno ilitwaa tiketi hiyo baada ya kuwazidia maarifa wapinzani wao Chuka University kwa kuibugiza mabao 3-2.
Susan Wanjeri alitingia Chuka mabao hayo nao Rebeca Nkirote, Hilda Wanjiku na Nasibo Ibrahim wa Isiolo Starlets kila mmoja alitupia kambani bao moja na kuisaidia kubeba umalkia wa ngarambe hiyo.
Kwenye nusu fainali Chuka University ilikomoa Ngakaa Talents mabao 2-1 nayo Isiolo Starlets ilidhalilisha Mabuu Queens kutoka Moyale kwa mabao 8-0.
Kando na kikosi hicho kutuzwa Sh200,000 pia kilijivunia Riziki Fatuma kutwaa tuzo ya mnyakaji bora.
WAPINZANI
Orodha ya timu ambazo zimefuzu kushiriki fainali za mwaka huu inajumuisha:Wiyeta Girls (Bonde la Ufa), Falling Waters Mkoa wa Kati, Beijing Raiders (Mkoa wa Nairobi), Isiolo Starlets (Mkoa wa Mashariki) na Kwale Ladies malkia wa taji hilo katika Mkoa wa Mombasa.
Mechi hizo ziliratibiwa kuandaliwa Mwezi Juni jini Mombasa lakini hali ya kuzuka kwa maambukizi ya virusi vya korona itafanya zisongeshwe mbele.
WAZAZI
Kwa jumla meneja huyo anashukuru wazazi wote kwa kumwaminia kuwa na wanao kwenye mechi hizo maana alilazimika kuchukua jukumu kuwaombea ruhusa.
”Kwa sasa nina imani tosha wazazi hao wameona kati ya matunda ya kushiriki mchezo wowote maana baada ya ufanisi huo kila mchezaji alituzwa simu yenye dhamana ya sh10,000,” alisema.
Anatoa mwito kwa wazazi wasiwe wanawazuia wanao nafasi ya kukuza talanta zao michezoni.