KINA CHA FIKIRA: Enyi watafiti, mada za kuzamia zi tele tusibane mawazo
Na KEN WALIBORA
JUMA lililopita nilifanya makosa makubwa katika safu hii ya Kauli ya Walibora.
Niliuita uwanja wa kimataifa wa ndege wa Abeid Amani Karume, uwanja wa Amani. Nilichanganya mambo na kuwakosea wengi.
Haikuwa makusudi. Dkt Mohamed Seif Khatib, mmiliki wa Zenj FM na Zenj TV na zamani Waziri wa Michezo nchini Tanzania, alikuwa wa kwanza kunisahihisha. Namshukuru sana kwa kunitilia kalafati.
Uwanja wa michezo wa Amani upo kisiwani Zanzibar, ila si uwanja wa ndege. Hapo ndipo mtangazaji wa kandanda mkongwe Ramadhani Ali alipokuwa akitangazia mpira katika idhaa ya Sauti ya Zanzibar kwa umahiri wa kupigiwa mfano. Baadaye Ramadhani Ali alienda zake kufanya kazi katika Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani, DW.
Nilipata fursa ya kuonana naye uso kwa macho nilipoenda DW mnamo mwaka 2001 kwa mafunzo ya taaluma ya utangazaji. Siku hizi Ramadhani Ali keshastaafu.
Nimeenda Zanzibar mara tumbi nzima, ila ni safari yangu ya mwisho ndipo niliona uwanja wa Amani nikiwa hewani, ndege ikiwa inajongeajongea kutua kwenye uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume.
Si mara ya kwanza kukosea kwenye safu hii. Nadhani kwamba mwanafunzi mahiri anaweza kuiandika tasnifu nzima ya uzamili au uzamifu (wengine husema uzamivu) kuhusu makosa ya Ken Walibora katika safu yake gazetini. Kama unadhani natania kumbuka pindi nilipoutaja uwanja wa michezo wa mjini Arusha kuwa Uwanja wa Sheikh Amani Karume. Hapo ndipo marehemu Mzee Abdallah Shamte, (mshairi hodari ambaye kafariki mwaka huu) aliniletea ujumbe wa kunisahihisha. Kanieleza kwamba hata alikuwa keshawahi kucheza kandanda kwenye uwanja huo siku za ujana wake.
Ninachosema leo ni kwamba nakutana na wanafunzi wanaotapatapa kuhusu mada za utafiti. Mada zi tele. Kwa kweli, mbali na makosa ya Ken Walibora, mtafiti anaweza kujadili vipengele mbalimbali vya makala ya safu hii ambayo imeendelea kila juma tangu 2016.
Kwa nini maoni yangu hupuuzwa tu na wanahabari hata nikiwaambia kwamba corona ya Kiswahili inaanza kwa herufi “k”? Na kama huku ni kujipigia upatu mno, basi acha niwapigie wengine upatu.
Mbona wasitokee wanafunzi wanaotathmini mchango wa makala ya wadau mahsusi kwenye safu za magazeti ya Kiswahili tokea kwa Walter Mbotela, Ruo Kimani Ruo, Clara Momanyi, Leonard Mambo Mbotela, Kimani Njogu wa enzi zile, pamoja na Henry Indindi, Wanderi Kamau, Ludovick Mbogholi, Bitugi Matundura na Enock Nyariki, Henry Mokua, Samuel Mukenya na Charles Wasonga? Utafiti hauwezi kuwa tu nafasi ya wanawake katika riwaya za Euphrase Kezilahabi.
Nani mathalani anaufufua mdahalo mkali sana wa kishairi uliozuka baina ya washairi wakongwe na ambao sasa wote wameenda njia ya marahaba, yaani Khamisi Chombo na Abdallah Shamte (nilimtaja hapo juu) na kwa upande wa pili waliotofautiana nao kama vile marehemu Hassan Mwalim Mbega. Mpaka leo sielewi kwa nini tafiti nyingi za Kiswahili zinakakania kutafiti “nafasi” ya kitu fulani katika kadhia kadha wa kadha.