Habari

Mitumba yapigwa marufuku

March 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imepiga marufuku uagizaji wa nguo zilizotumika, almaarufu mitumba, kama sehemu ya mikakati ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Waziri wa Biashara na Ustawi wa Kiviwanda Betty Maina alisema kando na kuokoa maisha ya Wakenya hatua hiyo inalenga kulinda viwanda vya kutengeneza nguo vya humu nchini.

“Serikali imesimamisha uagizaji wa nguo za mitumba mara moja kulinda maisha ya Wakenya na kupiga jeki viwanda vya nguo nchini wakati huu wa janga la virusi vya corona,” Bi Maina akasema kwenye ukurasa wa akaunti ya Twitter ya wizara yake.

Marufuku hii ambayo inaathiri wafanyabiashara wengi wa mitumba nchini, imejiri saa chache baada ya Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kutangaza kuwa idadi ya watu walioambukizwa nchini imepanda hadi 25.

Hii ni baada ya watu wengine tisa kugunduliwa kuwa na virusi hivyo kufikia Jumanne.

Akiongea na wanahabari katika makao makuu ya Wizara ya Afya, Jumba la Afya House, Nairobi Bw Kagwe alisema visa vya maambukizi vimeathiri zaidi kaunti za Nairobi, Mombasa, Kilifi na Kwale.

“Watu hao tisa, saba kati yao wakiwa Wakenya na wawili wageni, wamezuiwa katika taasisi za serikali zilizoidhinishwa na wanahudumiwa na wataalamu wa kiafya. Wale walioambukizwa awali wako katika hali nzuri,” akasema Bw Kagwe.