• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Olimpiki zaahirishwa kwa muda sababu ya maradhi ya Covid-19

Olimpiki zaahirishwa kwa muda sababu ya maradhi ya Covid-19

Na MASHIRIKA

TOKYO, JAPAN

MICHEZO ya Olimpiki iliyofaa kuandaliwa jijini Tokyo, Japan kati ya Julai 24 hadi Agosti 9, 2020 imeahirishwa kutokana na hofu ya kuenea zaidi kwa maambukizi ya homa kali ya virusi vya corona.

Hadi kufikia Jumanne zaidi ya watu 350,000 walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo, vifo 15,000 vikiripotiwa na takriban watu wengine 100,000 wakiendelea kupata nafuu.

Ishara za kufutiliwa mbali kwa Olimpiki za Tokyo zilitolewa mapema na mataifa ya Canada na Australia yaliyojiondoa katika michezo hiyo na kuwa nchi za kwanza kuchukua hatua hiyo.

Kamati ya Olimpiki ya Canada ilisema kuwa ilifikia “uamuzi mgumu” wa kuondoa wanamichezo wake baada ya kushauriana nao, mashirika ya spoti na serikali ya Canada. Kisha ikatoa “wito wa dharura” kwa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), ile ya Olimpiki za Walemavu na Shirika la Afya Duniani (WHO), kuahirisha michezo hiyo kwa mwaka mmoja zaidi.

Awali, IOC ilikuwa imesisitiza kwamba Olimpiki za mwaka huu hazingefutiliwa mbali huku vinara wake wakipendekeza kupunguzwa kwa idadi ya fani ambazo zingeshirikishwa.

Mara ya mwisho kwa michezo ya Olimpiki kufutiliwa mbali ilikuwa 1940 kutokana na vita vya Pili vya Dunia. Olimpiki za mwaka huo zilikuwa iandaliwe tena jijini Tokyo, Japan.

Kuahirishwa kwa Olimpiki za mwaka 2020 badala ya kufutiliwa mbali kabisa, ni afueni tele kwa Japan ambao tayari wametumia takriban Sh30 bilioni kufanya maandalizi.

Kuahirishwa kwa Olimpiki za Tokyo ni zao la presha ambayo imekuwa ikitolewa na watu, mashirikisho, na mataifa wanachama kwa IOC ambayo yamekuwa yakitaka michezo hiyo kuandaliwa baada ya virusi vya corona kudhibitiwa kabisa kote duniani.

Mwanzoni mwa wiki hii, mwenyekiti mpya wa Shirikisho la Riadha la Uingereza, Nic Coward, alipendekeza kuahirishwa kwa Olimpiki kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

Wito wa Coward ulitolewa baada ya kufutiliwa mbali kwa takriban matukio yote katika kalenda ya spoti za kimataifa mwaka 2020.

“Kuendelea na mipango ya kuandaa michezo hiyo wakati ambapo dunia inazidi kutikiswa na homa kali ya corona ni hatari. Ipo haja kwa mipango hiyo kutathminiwa upya na mwafaka kupatikana,” akasema Coward.

Akihojiwa na gazeti la The Sun nchini Japan, Mkurugenzi wa Shirikisho la Taekwondo la Uingereza, Gary Hall, alisema uwezekano wa kuandaliwa kwa Olimpiki za Tokyo mnamo Julai ulikuwa wa asilimia 50-50 hadi kufikia Jumatatu.

Mbali na Coward na Hall, wengine ambao walitaka michezo ya Olimpiki za 2020 kuahirishwa ni vinara wa kamati za mashindano hayo nchini Norway, Slovenia na Amerika.

You can share this post!

Mitumba yapigwa marufuku

RIZIKI: Athari za Covid-19 kwa wafanyabiashara

adminleo