• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
RIZIKI: Athari za Covid-19 kwa wafanyabiashara

RIZIKI: Athari za Covid-19 kwa wafanyabiashara

Na SAMMY WAWERU

KABLA kisa cha kwanza cha maambukizi ya Covid-19 kuripotiwa nchini Kenya mapema Machi, Simon Kagombe ambaye ni mfanyabiashara katika soko la Jubilee kiungani mwa jiji la Nairobi anasema alikuwa akipokea mapato ya kuridhisha.

Biashara ingedorora, asingekosa kufanya mauzo ya nguo zisizopungua nane kila siku.

Biashara inaponoga, Simon alikuwa akiuza zaidi ya mavazi 30 kwa siku.

“Biashara ndiyo mwajiri wangu, ndiyo hunikithi mahitaji yangu na ya familia na kujiendeleza kimaisha,” anadokeza.

Hata hivyo, hali si hali tena. Simon anasema kisa cha kwanza cha maambukizi ya virusi hatari vya corona kiliporitiwa nchini, mauzo yalianza kupungua. Ongezeko la visa vinavyoendelea kutangazwa, ndivyo mauzo yanazidi kushuka.

Kufikia sasa Kenya imethibitisha kuwa na maambukizi 25 ya Covid-19 na mfanyabiashara huyo analalamika kukadiria hasara.

Simon ameiambia ‘Taifa Leo’ kwamba ni kwa neema za Mungu kuuza nguo mbili kwa siku.

“Inanichukua hadi siku mbili mfululizo kuuza idadi hiyo,” akasema.

Wakati wa mahojiano, mfanyabiashara huyo alisema katika mavazi anayouza, long’i za jinsia ya kike na kaptura, “zimelala kwenye ghala”.

“Katika biashara bidhaa kusalia kwenye stoo kwa muda mrefu ni hasara. Hizo ni pesa zimelala ilhali zinapaswa kuwa zikisambaa kwenye uchumi”.

Kwenye kibanda kingine katika soko hilo la Jubilee lililoko mtaani Githurai, tunakutana na Dennis Mutua, ambaye ni muuzaji wa taweli, mapazia na mashuka. Kilio ni kilekile, “mauzo yameshuka na anachokadiria ni hasara tupu”.

“Biashara zimedorora kabisa tangu janga la Covid – 19 litangazwe nchini. Nilikuwa na vijana kadhaa wa kazi, wanashinda siku nzima bila kufanya mauzo, hawapati mshahara kwa kuwa huwalipa kulingana na kiwango ya mauzo,” Mutua analalamika. Mfanyabiashara huyo anasema siku anazobahatika kufanya mauzo ni chache mno.

Licha ya mikakati ya soko hilo kuimarisha kiwango cha usafi kwa njia ya maji yenye dawa na jeli kunawa mikono, wafanyabiashara wanalia wateja wamepungua kwa kiasi kikuu.

Mtungi wa maji yaliyotibiwa katika soko la Jubilee. Picha/ Sammy Waweru

Baadhi ya vibanda vimesalia kufungwa, ikikumbukwa kuwa wanatozwa ada ya kanju kila siku. “Imekuwa vigumu kulipia ada ya kanju ilhali hatufanyi mauzo,” anasema mfanyabiashara Reginah Wairimu.

Kwa mujibu wa wafanyabiashara tuliozungumza nao katika soko hilo, wamedai ilani ya biashara kufungwa kuanzia Ijumaa imetolewa. Masoko ya Thika yalifungwa mnamo Jumanne.

Huku serikali ikiendelea kuhamasisha umma jinsi ya kudhibiti Covid – 19 na kuweka mikakati kabambe, imeonya taifa litarajie kipindi kigumu na kuathirika kwa kiwango cha uchumi kufuatia virusi hivyo hatari.

 

  • Tags

You can share this post!

Olimpiki zaahirishwa kwa muda sababu ya maradhi ya Covid-19

Wakenya walionunua tiketi za Olimpiki 2020 kujua hatima yao...

adminleo