• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
Wakenya walionunua tiketi za Olimpiki 2020 kujua hatima yao wiki chache zijazo

Wakenya walionunua tiketi za Olimpiki 2020 kujua hatima yao wiki chache zijazo

Na GEOFFREY ANENE

WANUNUZI wa tiketi ya michezo ya Olimpiki 2020 iliyoratibiwa kuandaliwa mjini Tokyo nchini Japan mnamo Julai 24 hadi Agosti 9, watafahamu wiki chache zijazo iwapo itawezekana kutumia tiketi hizo baada ya mashindano hayo kuahirishwa hadi mwaka 2021.

Wateja wengi walionunua tiketi hizi wakiwemo maelfu ya Wakenya, wamekuwa na hamu kubwa kufahamu iwapo tiketi hizo zitatumika ama wataishia kupoteza fedha zao kutokana na hatua ya Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) na waandalizi Japan kuamua kuisukuma mbele kwa sababu ya hofu ya virusi hatari vya corona, ambavyo vimeua karibu watu 20, 000 kote duniani.

Mwandishi huyu aliuliza kampuni ya Kingdom Sports Group, ambao ni wauzaji wa tiketi hizo katika mataifa 36, swali hilo. Ingawa hakupata jibu, kampuni hiyo ilijibu mashabiki waliouliza swali hilo kwenye mtandao wake wa Facebook kwa kusema, “Tunasubiri jibu kutoka kwa wenyeji Tokyo na kamati ya IOC. Watatuthibitishia wiki chache zijazo. Kwa sababu michezo imeahirishwa na wala haijafutiliwa mbali, tunaamini kuwa hakuna kitu kitabadilika isipokuwa tarehe za mashindano tu. Hata hivyo, tutapata mwelekeo kutoka kwa wenyeji Tokyo na sera watakazoagiza tufuate.”

Majibu hayo yanaonekana hayakuridhisha shabiki mwingine ambaye alitaka kufahamu kama wanunuzi watarejeshewa fedha zao “kwa sababu wengine hawatafaulu kusafiri Tokyo katika tarehe mpya zitakazotolewa.” Alijibiwa,“Mashindano yameahirishwa na wala hayajafutiliwa mbali kwa hivyo tutapata mwelekeo kutoka kwa waandalizi na IOC. Tunatarajia uamuzi ufanywe wiki chache zijazo, lakini kwa wakati huu hatuwezi kutoa ushauri kuhusu hali ya kila mtu aliyenunua tiketi pamoja na maswali kuhusu tarehe mpya. Mara tu tutakapofahamu tarehe mpya, tutawapatia ushauri unaofaa.”

Mnamo Machi 16, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Daniel Beniston alieleza mwandishi huyu kuwa Wakenya walikuwa na shughuli nyingi katika kununua tiketi siku hiyo, ambayo ndiyo ilikuwa ya mwisho ya kupata tiketi za michezo hiyo inayofanyika kila baada ya miaka minne. Inamaanisha kuwa Wakenya wengi walinunua tiketi hizo na watakuwa katika orodha ya wanunuzi watakaosubiri kwa hamu kubwa kujua iwapo watapata afueni ya kurudishiwa fedha zao ama kuhudhuria michezo hiyo mwaka 2021 bila ya kulipia tiketi upya. Bei ya tiketi za mwisho kuuzwa hapo Machi 16 ilikuwa kati ya Sh2,995 na Sh136, 362 kila moja kutegemea na siku ya mashindano, fani anayotaka kuona na ukumbi/uwanja utakaotumika.

Wanamichezo 87 wa Kenya wamefuzu kushiriki michezo hiyo ya kifahari wakitoka katika fani ya raga ya wachezaji saba kila upande wanawake (Lionesses) na wanaume (Shujaa), wanamasumbwi wawili (mmoja mwanamume na mwingine mwanamke), taekwondo (mwanamke), uogeleaji (tiketi mbili), timu ya voliboli ya ukumbini ya Malkia Strikers (wanawake), timu ya riadha (wanaume kwa wanawake) na mpigaji wa makasia mmoja mwanamke atakayeshiriki Olimpiki za walemavu.

You can share this post!

RIZIKI: Athari za Covid-19 kwa wafanyabiashara

KAFYU: Maisha magumu yaanza

adminleo