'Wachezaji wa raga waliombaka msanii wakamatwe'
GEOFFREY ANENE
MWENDESHA mashtaka mkuu wa Kenya ameamrisha kukamatwa na kushtakiwa kwa wachezaji wawili wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande waliotuhumiwa kwa ubakaji, shirika la habari la Capital FM limeripoti Ijumaa.
Wachezaji hao Frank Wanyama na Alex Olaba kutoka klabu ya Kenya Harlequins wanatuhumiwa kumbaka mwanamuziki Wendy Kemunto mnamo Februari 10, 2018 katika jumba moja mtaani Kilimani jijini Nairobi.
Kupitia mtandao wake wa Instagram, Kemunto alidai Wanyama na rafiki yake walimbaka wakibadilishana siku yake ya kuzaliwa Februari 10 na kumuacha akiwa mjamzito.
Kemunto hakutaka kupiga ripoti kwa polisi kuhusu kisa hiki akihofia hakitachukuliwa kwa uzito, lakini baada ya kuenea kwenye mitandao ya kijamii, habari hizo zilifikia afisi ya Mwendesha mashtaka mkuu wa Kenya na akaahidi kuchunguza kesi hiyo hadi haki itendeke.
Kitengo cha ujasusi kimefanya uchunguzi wake na kutoa taarifa Ijumaa kwamba wachezaji hao watiwe nguvuni na kushtakiwa. Tovuti ya Capital FM imesema kwamba mwanamuziki huyo alidai alipewa dawa za kumfanya apoteze fahamu na wachezaji hao na kisha kushawishiwa kuingia katika nyumba moja na kubakiwa humo.
Harlequins ilithibitisha Aprili 3 kwamba ilipokea malalamishi kuhusu wachezaji hao ambao imeajiri. Iliongeza, “Kama mojawapo ya klabu kongwe nchini na inayoheshimika, tunafuata sheria za maadili zinazostahili kufuatwa kikamilifu na wachezaji na maafisa wa klabu. Kenya Harlequins pia haikubali kabisa tabia ya aina yoyote ya unyanyasaji wa kimapenzi,” klabu hiyo ilisema.
Kulingana na tovuti ya Shujaa Pride, Wanyama, ambaye jina lake la utani ni ‘Animal’ ama ‘magician’, alizaliwa Oktoba 20 mwaka 1994 na kujiunga na Shule ya Upili ya Nakuru High kabla ya kusomea “Actuarial science” katika Chuo Kikuu cha Strathmore na Sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Olaba, ambaye alisomea Shule ya Upili ya Alliance, ni mchezaji wa zamani wa klabu ya Strathmore Leos.