• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:50 AM
AKILIMALI: Mmea wa viazi vikuu ni rahisi kukuza maeneo kame kama vile Ukambani

AKILIMALI: Mmea wa viazi vikuu ni rahisi kukuza maeneo kame kama vile Ukambani

CORNELIUS MUTISYA na CHARLES WASONGA

NI jambo la kutia fora sana kuwaona wakulima kutoka janibu za Ukambani wakizua mbinu na mikakati kabambe ya kukabiliana na baa la njaa ambalo limekumba eneo hilo miaka nenda miaka rudi.

Wakulima hao wameingilia kilimo cha mimea inayohimili ukame kama vile mihogo, mawele, mtama na hata viazi vikuu almaarufu nduma. Si shani kwamba, bidii yao ya mchwa imezaa matunda mema na ya kuonewa fahari.

Katika kitongoji duni cha Kiliku, kata ya Iveti, Kaunti ya Machakos, mwanakijiji mmoja ambaye ametambua fika kwamba, kilimo ndicho chanzo cha kupunguza janga la njaa janibu za Ukambani.

Huyu sio mwingine ila Mzee Muindi Muasya, ambaye amekuza mazao ya kustahimili ukame kama vile nduma na mihogo katika shamba lake la ukubwa wa ekari moja.

“Mimi hukuza nduma katika shamba nililorithi kutoka kwa wazazi wangu. Janga la njaa kwangu ni kama hekaya za abunwasi,’’ asema Muasya, maarufu mitaani kwa jina, ‘Kanzi.’

Anasema ya kwamba, siri ya ufanisi wake katika kilimo cha nduma ni kuwa hufuata kikamilifu maagizo bora ya maafisa kilimo kuhusu mbinu za kisasa.

“Nilitambua fika kuwa mmea wa nduma hauhitaji mambo mengi. Ukitia rotuba vizuri, unaweza kuvuna mazao baada ya muda wa kati ya miezi sita na minane,’’ anasema Muasya.

Aidha, mkulima huyu aarifu ya kwamba, nduma huwa na faida kubwa adhimu katika mwili wa binadamu.. Ina utajiri wa madini muhimu kwa mwilini, kama vile, Thiamin, Oflavin, Iron, Phosphorus, Vitamin B, Zinc.

Kwa wastani, mkulima huyu hutia kibindoni kati ya Sh70, 000 na Sh100,000 kwa mwaka kutokana na kazi hiyo, baada ya kuondoa gharama nyinginezo.

“Huwa nauza mazao yangu kwa viwango vya jumla na rejareja. Soko yangu kuu ni mikahawa mikubwa katika miji ya Machakos na Nairobi,” anasema.

“Na baadhi ya wateja wangu huja shambani kununua viazi vikuu ambapo huwa nauza kilo moja kwa Sh100 kwa bei ya jumla. Wateja ambao hawaendi kuuza nao huwa nawauzia kilo ya nduma kwa Sh150, ” Muasya anafafanua.

Anasema mojawapo ya manufaa ya kilimo cha nduma ni kwamba huwa haina msimu wa mavuno, huvuna na kuuzwa nyakati zote inapokomaa.

Aidha, Muasya anayekuza pia mihogo asema alipoona baa la njaa likikumba eneo hilo miaka minane iliyopita ndipo anakumbatia kilimo hicho

Kwa hivyo, anawashauri wakulima wa eneo kukumbatia kilimo cha mimea inayostahili ukame kando na mimea mingine cha mahindi na maharagwe.

Changamoto zinazomkabiliwa katika kilimo hicho ni gharama ya kununua dawa za kunyunyiza ili kuangamiza wadudu waharibifu.

Vilevile, baadhi wa wateja huwa wasumbufu kwa sababu hununua kwa deni na kukawia kulima,” Muasya anasema.

  • Tags

You can share this post!

AKILIMALI: Mbuzi wa nyama wamletea faida kuliko wa maziwa

CORONA: Wachuuzi wafurushwa

adminleo