Corona yalazimu mbio za vijana duniani kuahirishwa

Na CHRIS ADUNGO

RIADHA za Dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 zilizokuwa zifanyike jijini Nairobi kati ya Julai 7-12, zimeahirishwa kutokana na hofu ya maambukizi ya virusi vya corona.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF), maamuzi hayo yaliafikiwa baada ya mashauriano ya kina na wahusika mbalimbali, pamoja na mashirikisho wanachama yaliyokuwa yashiriki mashindano.

Kufikia sasa, serikali za nchi nyingi duniani zimesitisha ziara za kimataifa huku zikiagiza raia wanaorejea kutoka nchi za kigeni kujitenga kwa siku 14 na kuepuka mikutano ya hadhara.

“Ilitulazimu kuzingatia afya na maisha ya wanariadha, maafisa na mashabiki. Tunatambua ukubwa wa viwango vya maandalizi yaliyokuwa yamefanywa na Kenya kwa minajili ya mashindano hayo, lakini kwa sasa imetubidi kusitisha mbio hizo kwa muda. Tarehe mpya itatolewa hivi karibuni,” ikasema taarifa ya IAAF.

Matabibu wa IAAF wanaoshirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), wanashikilia kwamba viwango vya kuenea kwa homa ya corona miongoni mwa mataifa mbalimbali ulimwenguni ni vya kutisha mno kwa sasa, na mojawapo ya njia kuu za maambukizi ni mikusanyiko ya umma.

Waziri wa Michezo Amina Mohammed, alipongeza hatua ya IAAF na serikali ya Japan ambayo pia iliahirisha Olimpiki za Tokyo 2020.

Riadha nyinginezo za dunia ambazo tayari zimeahirishwa ni ile ya Indoor Championships mjini Nanjing, China; Nusu Marathon ya Dunia mjini Gdynia, Poland na Matembezi yaliyokuwa yaandaliwe mjini Minsk, Belarus.

Nchini Kenya, mamia ya wanariadha tayari wamesimamisha mazoezi katika kambi 20 za mazoezi zilizoko Kaunti ya Nandi kutokana na virusi vya corona.

Akieleza baadhi ya hatua ambazo serikali ya Kaunti ya Nandi imechukua kukabiliana na corona, Gavana Stephen Sang alisema kambi za wanariadha ni tishio kubwa katika kukabili corona.

“Tuna makocha, mameneja, mawakala wa kigeni na wanariadha wengi ambao husafiri mara kwa mara ndani na nje ya nchi. Hivyo, tumeamua kufunga kambi zote za wakimbiaji kwa kipindi cha siku 30 zijazo,” akaamuru Sang.

Habari zinazohusiana na hii

Leave a Reply