• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
KILIMOMSETO: Barobaro aliyerithi kilimo kutoka kwa wazazi sasa avuna donge

KILIMOMSETO: Barobaro aliyerithi kilimo kutoka kwa wazazi sasa avuna donge

CORNELIUS MUTISYA na BENSON MATHEKA

ALIRITHI kilimo kama ajira kutoka kwa wazazi wake na akaamua kuwa mkulima maishani. Amesomea masuala ya kilimo katika chuo kikuu na akazama kwenye zaraa hii kikamilifu.

Ni mmoja wa vijana wanaoamini kilimo ndicho uti wa mgongo katika ufanisi wa jamii na taifa lolote lile. Tunazungumzia Lazarus Peter, mkulima mashuhuri wa mimea mbalimbali na mfugaji stadi wa wanyama wa kila sampuli janibu za ukambani.

Amekumbatia kilimo mseto ili kujikinga na hali yoyote inayoweza kuzuka.

“Katika kilimo mseto, mtu hawezi kupata hasara kubwa sana kwa sababu akikosa kufanikiwa katika zao moja, anafaulu kwa lingine, akikosa kufanikiwa kwa mazao, anafaulu katika ufugaji. Kuna manufaa tele,” asema.

Lazarus aliye mzaliwa wa kitongoji cha Kaliluni, Lokesheni ya Iveti, kaunti ndogo ya Kathiani amezoa sifa kochokocho kutokana na kilimo cha avakado na mahindi.

Pia ni mfugaji stadi wa ng’ombe wa maziwa, sungura, kuku na nguruwe na huwa anahusika na upanzi wa miche.

Mkulima huyu bomba alianza kujishughulisha za zaraa ya kilimo tangu utotoni mwake. Alikuwa anaandamana na wazazi wake, marehemu Peter Nzuki na Monicah Nzuki, waliokuwa wakulima shupavu kwenda kupalilia shamba lao baada ya kutoka shule majira ya jioni.

Asema kwamba, aliingilia rasmi shughuli za kilimo mwaka wa 2012 alipohitimisha masomo yake katika chuo cha South Eastern Kenya University alipopata Diploma katika kilimo.

”Nilianza kulima mazao kama nduma na nyanya. Kilimo hiki kilifaulu mno hadi nikawa mfano mwema wa kuigwa na vijana wa janibu za Ukambani,” asema Lazarus.

Asema kwamba, akiwa na wazazi wake alikuwa anaenda kuuza nyanya hizo kisiwani Mombasa katika soko maarufu la Kongowea, nazo nduma walikuwa wanasambaza katika mahoteli makubwa makubwa mjini Machakos.

”Nilipata donge nono kutokana na kilimo hicho. Niliamua kutolegeza jitihada zangu asilani,” asema barobaro huyu huku akitabasamu.

Mwaka wa 2014, alikata kauli kupanua kilimo chake na akaanza ufugaji wa kuku na nguruwe. Hii ilikuwa baada ya wazazi wake kuaga dunia Sifa zake zilitanda kote mithili ya cheche za moto nyikani na ndipo mapato yake yalivyoongezeka.

” Sifa zangu zilivuma kote hadi maafisa wa kilimo nyanjani wakaanza kunitembelea mara kwa mara. Walinihimiza nipeleke baadhi ya nduma zangu katika maonyesho ya kilimo ya mjini Machakos,” asema.

Mnamo 2016, alipeleka nduma zake katika maonyesho ya kilimo mjini Machakos. Alikabidhiwa cheti cha mkulima bora kijijini.

Asema kwamba, katika upanzi wa miche, huwa anatia kibindoni zaidi ya Sh70 00 wakati wa msimu wa mvua. Katika kilimo cha avakado huwa anapata faida ya sh 50, 000 kwa msimu mara nne kwa mwaka. Hivyo, kwa mwaka huwa anapata Sh200,000 kwa kuuza parachichi pekee.

Hata hivyo, hakuna masika yasiyo na mbu. Licha ya kupata ufanisi maridhawa katika kilimo, barobaro Lazarus huwa anakabiliwa na changamoto kadha.

Hii ni kwa sababu wakati mwingine bei ya mazao yake huwa duni masokoni na hivyo kupunguza mapato yake.

Kwa mintarafu hii, Lazarus anaomba serikali ya Kaunti ya Machakos kupitia idara ya kilimo ipike jeki wakulima wakati wa hali ngumu ya kiuchumi pamoja na kuwasaidia kupanua shughuli zao.

  • Tags

You can share this post!

Masoko Ruiru kufungwa kwa siku 21 kuzuia kuenea kwa Covid-19

COVID-19: Maspika wakubali makato ya asilimia 30 ya...

adminleo