COVID-19: Maspika wakubali makato ya asilimia 30 ya mishahara yao
Na DAVID MWERE
SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Ken Lusaka wamekubali makato ya asilimia 30 ya mishahara yao kukabili maradhi ya Covid-19.
Kufikia Alhamisi adhuhuri, wabunge na maseneta walikuwa bado kukubaliana kuhusu ama kukubali au kukataa makato ya mishahara yao.
Notisi katika gazeti rasmi la serikali iliyotolewa na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) Julai 2017 inabainisha maspika wa Bunge la Kitaifa na Seneti wanafaa kupokea mshahara wa Sh1,155,000 kila mwezi kwa kila mmoja.
Hatua ya hawa wawili sasa inamaanisha Bw Muturi na Bw Lusaka watapokea Sh805,500 kila mmoja kwa muda wa miezi miwili ijayo.
Kabla ya kufikia uamuzi huo walihitaji kuiandikia SRC kuieleza wananuia makato ya asilimia fulani kutekelezwa kwa mishahara yao.
Inatarajiwa SRC itawasilisha mapendekezo yao kwa Wizara ya Fedha.
“Tumewaandikia makatibu wa mabunge haya mawili kuziandikia asasi husika za serikali kutekeleza mapendekezo yetu ili makato yaelekezwe kwa vita dhidi ya Covid-19,” amesema Bw Lusaka.
Jumatano Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kwamba yeye na Naibu Rais William Ruto wamekubali makato ya hadi asilimia 80 ili pesa zipatikane za kutumika kukabiliana na maradhi ya Covid-19.
Kiongozi wa nchi alitangaza pia mawaziri watakatwa asilimia 30 kila mmoja huku makatibu katika wizara wakikatwa asilimia 20 ya mishahara yao kila mmoja.
Mawaziri sasa watapokea Sh646,000 kila mmoja nao makatibu wakipokea Sh612,150 kila mmoja kwa kila mwezi katika kipindi hiki kigumu.