COVID-19: Gavana azuru hospitali tatu za kaunti ya Kiambu kujionea maandalizi
Na LAWRENCE ONGARO
GAVANA wa Kiambu amezuru hospitali tatu kuu za kaunti hiyo na kuridhika na jinsi ambavyo wamejiandaa kupambana na Covid-19.
Dkt James Nyoro, alizuru hospitali ya Kiambu Level 5, Thika Level5, na Gatundu Level 5 na kupata ya kwamba wamejiandaa kukabiliana na jambo lolote litakalofika mbele yao.
Kila hospitali imetenga wadi ya wagonjwa wa Covid-19 huku pia wauguzi wakipewa mafunzo jinsi ya kukabiliana na janga hilo.
Wakati wa ziara yake mnamo Alhamisi, aliandamana na maafisa wakuu katika kaunti hiyo huku pia akipimwa halijoto ya mwili.
Alisema kaunti ya Kiambu imeongeza kiwango cha Sh 40 milioni kukabiliana na janga hilo la homa ya corona.
“Nimeridhika na jinsi madaktari katika hospitali hizo tatu wamejiandaa kukabiliana na janga hilo. Ni sharti tuungane kukabiliana na janga hilo. Ni vyema kuungana pamoja kupambana nayo,” alisema Dkt Nyoro.
Alitoa mwito kwa wananchi kuzingatia usafi kwa kunawa mikono na kuhakikisha wanajitenga na umati mkubwa.
Wakati huo pia wasafiri wengi waliachwa na mshangao huku magari za usafiri zikipandisha nauli kiwango cha juu.
matatu za Thika-Ruiru zinatoza Sh 80 badala ya Sh 50. Halafu zile za Thika-Nairobi zinatoza 150 badala ya Sh 100.
Hata hivyo ni wasafiri wachache ndio wanaoabiri matatu hizo kwa sababu wengi walifunga kazi wiki moja iliyopita.
Lakini wamiliki wa matatu pia wanasema ya kwamba kwa sababu wanabeba wasafiri wachache ni sharti wafanye hivyo ili angalau kuweka hesabu iwe sawa kidogo.
Nao wahudumu wa Tuk-Tuk walilazimika kubeba abiria wawili badala ya wanne jinsi walivyozoea kubeba.
Polisi pia walitembelea vituo vya magari mjini Thika wakitaka kukagua kama kweli kila sehemu inatumia dawa ya sanitaiza kunawisha wasafiri.
Maeneo ya burudani na vyakula yalibaki mahame huku wateja wengi wakiamua kubaki nyumbani.
Michael Kamakis ambaye anamiliki eneo kubwa la burudani na vyakula katika mji wa Ruiru By-Pass alisema wateja wake wengi walikosa kufika katika maskani hiyo.
“Wakati mwingi eneo hili hujaa hadi pomoni hasa wikiendi, huku wateja wakila nyama choma na kujiburudisha na vinywaji,” alisema Bw kamakis.
Alikiri ya kwamba kwa wiki moja iliyopita amekwenda hasara kubwa ajabu lakini atalazimika kuvumilia hayo.
Mfanyi biashara mwingine Willy Mwangi alisema wafanyi kazi wake wengi wamekosa kazi ya kufanya na kubaki manyumbani.
“Hatutakuwa na jingine ila kumweka Mungu mbele. Sisi wenyewe hatuna uwezo kufanya lolote, kama binadamu ,” alisema Bw Mwangi.
Wakati huu wananchi popote walipo wanajaribu kurafakari jinsi amri ya kafyu itaadhiri shughuli zao kutoka leo Ijumaa huku wahudumu wa matatu wakirafakari jinsi watafika nyumbani mapema kabla ya saa 12 za jioni.