• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
AKILIMALI: Dobi anayehakikishia wateja huduma muda wa saa 24

AKILIMALI: Dobi anayehakikishia wateja huduma muda wa saa 24

Na MAGDALENE WANJA

BI Maurine Wanjiku aligundua umuhimu wa udobi alipokuwa akifanya kazi katika sekta ya hoteli.

Aliona jinsi ambavyo wateja wengi walikuwa wakisaka huduma ya usafishaji wa nguo na pia kupigiwa pasi ili kuzilainisha.

Alizungumza na ‘Taifa Leo’ mapema Machi ambapo alikiri katika sekta ya hoteli huduma za usafishaji zilizokuwa zikipatikana zilikuwa ghali sana kwa watu wa mapato madogo.

“Baada ya kufanya utafiti zaidi, niligundua kwamba watu wengi ambao walihitaji huduma hiyo walikuwa hawawezi kugharimia na nikaamua kuwekeza katika biashara hiyo ili nitoze ada nafuu,” akasema Bi Wanjiku.

Baada ya miezi miwili katika kazi yake ya awali, aliamua kuacha na kuanza kuifanya ile ya udobi.

“Mwaka 2018 niliagiza mashine ambayo ilitumia nishati ya kiwango cha chini na iliniwezesha kulipisha wateja wangu ada nafuu,” akaongeza dobi huyu.

 

Mwanzilishi wa biashara ya udobi ya Express DryCleaners Bi Maurine Wanjiku apiga pasi ofisini katika jengo lililo kando ya barabara ya Ngong, Nairobi Machi 6, 2020. Picha/ Kanyiri Wahito

Alizindua programu ya simu kwa jina Express Dry-Dleaners ambayo iliwawezesha wateja wake kumpata kwa urahisi; hasa katika mitandao ya kijamii.

“Katika wiki za mwanzo nilikuwa na wateja kati ya 10 na 15 ambao walitaka huduma za kufuliwa nguo kwenye mashine,” alisema Bi Wanjiku.

Hata hivyo, anasema, hakufa moyo kwani aliendelea na kazi hiyo mpaka alipopata wateja wengi.

Kufikia sasa, duka lake lililoko katika eneo la Ngong Road linafanya kazi kwa muda wa saa 24 na hivyo kumwezesha kuwahudumia wateja wake.

Bi Wanjiku anasema kuwa anapata oda kati ya 800 na 1,000 kwa siku huku malipo yake yakiwa ni kati ya Sh10 na Sh1,000.

You can share this post!

UMBEA: Kumpenda mtu kwa dhati kunahitaji mbinu na mikakati

TAHARIRI: Wanaspoti wakae fiti katika janga hili

adminleo