Wanaougua corona sasa wafika 50, wanabodaboda waonywa
NA FAUSTINE NGILA
WAZIRI wa Afya Bw Mutahi Kagwe Jumatatu ametangaza visa vipya 8 vya virusi vya corona na kufikisha 50 idadi kamili ya walioambukizwa humu nchini.
Alifichua kuwa maambukizi mapya yanatokana na usafiri wa bodaboda, ambao upo katika kila kona ya nchi.
Akiwarai Wakenya kuzidi kujikinga dhidi ya virusi hivyo, Bw Kagwe alitoa kanuni mpya kwa waendeshaji wa bodaboda ili kuzuia maambukizi kati yao na wateja wao.
“Wanabodaboda wabebe abiria mmoja kuanzia leo. Dereva na abiria wake wavae barakoa. Serikali itasambaza barakoa hizi katika kila kaunti,” akasema waziri huyo.
Alisema kuwa kwa watakaokaidi kanuni hiyo watalazimishwa na maafisa wa polisi.
“Polisi watatumika kuhakikisha kuwa sheria hii inafuatwa kwa kuwa wanabodaboda hubeba abiria wengi kila siku na huwezi kujua aliyeambukizwa na asiyeambukizwa,” alieleza.
Waziri huyo pia aliwaomba waajiri na kampuni kuwaruhusu wafanyakazi kutoka kazini kabla ya saa kumi alasiri ili wapate muda wa kufika kwao kabla ya kafyu.
Pia, aliwataka wanaoishi Nairobi wakome kusafiri mashambani ili wasiwaambukize wakongwe.
“Kama unawapenda wazazi na wakongwe walio mashambani, taafadhali ishi ulipo, usisafii. Walio mashinani pia msisafiri Nairobi au miji mingine,” alishauri Bw Kagwe.
Alifafanua kuwa safari za ndege zinazoruhusiwa katika anga ya Kenya ni zile za mizigo muhimu kama vifaa vya afya.
“Hakuna abiria wapya kutoka ng’ambo wanasafiri humu nchini. Pia, kutakuwa na ndege za kuwasafirisha raia wa kigeni kutoka humu nchini hadi mataifa yao,” alisema.
Alitaja kuwa Kenya sasa ina vifaa 20,000 vya kupima virusi hivyo huku vingine vikitarajiwa kuletwa nchini.
“Tunavikagua kuhakikisha ni halisi,” alisema waziri huyo.