Maisha magumu kwa wahudumu wa tuktuk
NA SAMMY WAWERU
Kabla ya kisa cha kwanza cha Covid – 19 kuripotiwa nchini Machi 13, 2020, Timothy Ndombi ambaye ni mhudumu wa tuktuk eneo la Githurai alikuwa akipata mapato ya kuridhisha.
Kwa siku, baada ya kuondoa gharama ya matumizi ambayo ni mafuta, mapato yakiwa ya chini mno hakuwa akikosa kuingiza kipato kisichopungua Sh1, 700.
“Kabla ya janga la virusi vya corona, siku bora mapato yalikuwa yakizidi Sh2, 500, gharama ya matumizi ikiondolewa,” Timothy ameambia Taifa Leo Dijitali kwenye mahojiano.
Hata hivyo, hali si hali tena. Kulingana na mfanyabiashara huyo, kwa sasa kufikisha mapato ya Sh1, 000 kwa siku ni kwa neema ya Mwenyezi Mungu. Biashara hiyo ya uchukuzi imeathirika kwa kiasi kikuu, wahudumu wakinyooshea kidole cha lawama mkurupuko wa Covid – 19.
Timothy ni mume na baba ya watoto watatu, na anasema hana kazi nyingine kukidhi mahitaji ya kimsingi ya familia yake ambayo ingali changa. Kila jioni, lazima aikimu riziki.
Tuktuk yake ni miongoni mwa mamia ya vijigari hivyo vidogo vinavyohudumu kati ya mtaa wa Githurai, Progressive, Mumbi na Mwihoko, mitaa iliyoko kiungani mwa jiji la Nairobi na inayoorodheshwa kuwa kaunti ya Kiambu.
Sekta ya uchukuzi, ni miongoni mwa biashara zilizopigwa dafrau na Covid – 19 na kuathirika pakubwa. Miongoni mwa taratibu na sheria zilizotolewa na serikali ili kudhibiti maenezi ya virusi vya corona, wahudumu wa matatu wametakiwa kushusha kiwango cha abiria wanaobeba mara moja, hadi asilimia 60 ya jumla ya idadi kamili.
Kwa mfano, matatu inayobeba jumla ya abiria 14, idadi hiyo imeshushwa hadi 8. Agizo hilo limelazimu wahudumu kuongeza nauli hadi mara dufu, wakijitetea “tumechukua hatua hiyo kukwepa kuenda hasara zaidi”.
Sawa na matatu, tuktuk pia zimetakiwa kufuata mkondo huo na kulingana na Timothy Ndombi, kila kijigari kinatakiwa kubeba abiria 3 kutoka jumla ya 5. Nauli kati ya Githurai hadi Mumbi huwa Sh20 kila abiria, na ada hiyo imepanda hadi Sh30 kufuatia mabadiliko yaliyofanywa.
Kwa mujibu wa wahudumu tuliozungumza nao, licha ya kuzingatia utaratibu na kanuni zilizotolewa, hasa kupunguza idadi ya abiria na kudumisha kiwango cha usafi cha hadhi ya juu, idadi ya watu wanaosafiri imepungua kwa kiasi kikuu. “Hata hao abiria watatu kwa awamu moja hawapatikani,” akasema Simon Muchangi, mhudumu.
Kwenye mahojiano, Simon aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba kwa muda wa siku tatu zilizopita alilazimika kuegesha tuktuk yake, kwa kile alitaja kama kukadiria hasara. “Kati ya Jumatatu hadi Jumatano nilikuwa naweka gari mafuta ilhali halinipi mapato,” akalalamika.
Alisema si ajabu kuzunguka barabarani kwa muda wa saa nzima bila kupata abiria yeyote. Majira ya asubuhi na jioni, watu wakielekea kazini na kurejea makwao ndio muda wanaoingiza mapato, ingawa wanasema ni ya chini mno.
Kwa madereva walioajiriwa, wanalipa nusu ya mshahara walioagana na mmiliki. “Ikiwa dereva anapaswa kulipa Sh1, 000 kwa siku, imepungua hadi Sh500. Mambo yamekuwa magumu, biashara imedorora,” akasema dereva mmoja.
Isitoshe, mbali na masaibu yanayowakumba, kafyu iliyoanza kutekelezwa Machi 27, 2020, imeathiri huduma zao kwa kiasi kikuu. Rais Uhuru Kenyatta aliagiza kafyu ya kila siku kuanzia saa moja za jioni hadi saa kumi na moja za asubuhi, ili kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi hatari vya corona.
Tuktuk nyingi zinalazimika kuegeshwa kwa sababu ya kukosa abiria. Inawachukua wahudumu muda kushawishi watu kusafiri nazo, wengi wakionekana kuhofia na kutembea kwa miguu ikiwa wanakoelekea si mbali. Eneo hilo lina zaidi ya tuktuk 300.
Alhamisi, akitahadharisha taifa kuhusu ueneaji zaidi wa Covid – 19 kwa alichotaja kama “umma kupuuza taratibu na sheria” zilizotolewa na serikali kudhibiti maambukizi, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amewataka madereva na abiria kuanza kuvalia barakoa ya kufunika mdomo na pua. “Ninaamuru madereva wa tuktuk na matatu pamoja na abira waanze kuvalia barakoa,” akaagiza Waziri Kagwe.
Waziri aidha amesema serikali imeanza harakati za kutengeneza barakoa, alizoahidi zitaanza kusambazwa baada ya siku mbili zijazo. Pia, amewataka wafanyabiashara wauzaji wa bidhaa hizo kuziuza kwa bei nafuu.