JAMVI: Wanasiasa wabuni njia za kijanja kujitangaza wakati huu wa virusi
Na BENSON MATHEKA
WANASIASA ambao wamezoea kutumia mikutano ya hadhara, mazishi na ibada makanisani kushambuliana kujipigia debe wanakabiliwa na wakati mgumu wakati huu ambao mikutano imepigwa marufuku kufuatia janga la corona.
Na sasa, baadhi yao wamebuni mbinu za kuhakikisha sauti zao hazififii kabisa kwa sababu ya kukosa majukwaa ya kuendeleza siasa zao.
Wadadisi wanasema kuwa marufuku ya mikutano ya hadhara, ibada na mazishi inahatarisha maisha ya siasa ya wanasiasa wengi ambao walikuwa wakiitumia kujipigia debe kwa kushambulia wapinzani wao.
“Tumeona wanasiasa wakiwa na wakati mgumu sana baada ya kukosa majukwaa ya kushambulia wapinzani wao. Kabla ya visa vya corona kuanza kuthibishwa nchini wiki tatu zilizopita walikuwa wakitumia mikutano ya hadhara, mazishi na makanisa kushambuliana hasa kuhusu siasa za urithi za 2022.
Wakati huu wanalazimika kubuni mbinu za kuhakikisha sauti zao zinasikika,” asema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.
Anasema wengi wao wanatumia mitandao ya kijamii njia ya pekee ya kufikia Wakenya kwa wakati huu. Katika juhudi za kudumisha umaarufu wao wamekuwa wakifanya vituko kwa lengo la kuvutia Wakenya.
“Kwa vile mada moto kwa wakati huu ni corona na ni suala la kufa kupona hata wanasiasa wenyewe, wamelazimika kuwa waangalifu wanapolizungumzia. Baadhi wanazua vituko wakijaribu kupaza sauti zao kulihusu.
Kwa mfano, seneta wa Nairobi Johnson Sakaja alilazimika kugeuza familia yake kuwa bendi ya muziki na kurekodi wimbo akiwa na watoto wake aliopakia kwenye mitandao ya kijamii kuwaonya watu kujilinda. Baadhi ya wabunge wamekuwa wakitoa misaada ya matangi ya maji na sabuni kwa wakazi ambao awali walikuwa wakiwalilia wawasaidie bila kufaulu.
“Kwa vile sasa hakuna mikutano ya wanahabari, kwa vile sasa hakuna majukwaa ya kujivumisha, wanasiasa wamelazimika kurejea mashinani ambako walikuwa wametelekeza wapigakura na kujifanya wanawasaidia kupigana na corona. Tumeona waliokuwa wamepuuza vilio vya wakazi kuhusu shida la maji wakitoa mapipa ya maji yaliyo na nembo ya picha zao. Hii ni mbinu ya kuwafanya wasikike tu,” asema Kamwanah.
Ilibidi maafisa wa utawala kupiga marufuku misaada ya wanasiasa wakisema wanaitumia kujipigia debe wakati wa janga hatari la corona.
Kulingana na kamishna wa kaunti ya Trans Nzoia Sam Ojwang wanasiasa hawana nia njema wanapotoa misaada ya vifaa vya kukabiliana na corona na kuwataka wanaotaka kuiwasilisha kwa kamati ya kukabiliana na dharura ya kaunti badala ya kuipeleka moja kwa moja kwa umma.
Kama mbinu ya kumfanya aendelee kusikika, mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro alitangaza kuwa atatoa mshahara wake wote kusaidia wakazi wa eneobunge lake wanaokabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi. Mbunge huyo ni mmoja wa wanachama wa kundi la Tangatanga linalounga Naibu Rais William Ruto na kupinga Mchakato wa Maridhiano (BBI).
Wadadisi wanasema hatua yake hiyo ni mbinu ya kudumisha sauti yake wakati huu ambao hakuna jukwaa la kuendeleza siasa kwa kuwasiliana moja kwa moja na umma.
Tangatanga lilikuwa likiandaa mikutano ya kuchangia makanisa na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo kujipigia debe.
“Kwa wakati huu wanasiasa wamebadilika kuwa mabloga. Wanaandika sana kwenye mitandao ya kijamii na kuchapisha picha wakiwa katika mashamba yao wakijifanya wanalima. Kusema kweli hawana la kufanya na kwa sababu wamezoea kuchapa siasa kuliko na watu wengi, sauti zao zinafifia,” asema mdadisi wa siasa Hilda Sambu.
Kwa sababu corona ni suala lisiloweza kufanyiwa mzaha wanasiasa walivyozoea, wamelazimika kuhubiri na kuahidi yasiyowezekana kama vile kusema watatengeneza na kugawa barakoa.
“Sisi sote tuvae barakoa kila siku tukiwa wagonjwa au la. Tusaidie tunavyoweza. Kwa upande wangu, nitatengeneza na kugawa barakoa kwa watu masikini katika kaunti yangu bila malipo,” alisema seneta mmoja kwenye Twitter. Kulingana na wataalamu ni lazima anayetengeneza barakoa atimize mahitaji fulani na viwango vya ubora na kauli ya seneta huyo lilikuwa la kisiasa pekee.
Wadadisi wanasema wanasiasa wamebanwa na maagizo ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona ndio sababu wanatumia mbinu tofauti kuhakikisha umaarufu wao haufifii.
“Hata wanaogopa kukutana wenyewe kwa wenyewe katika makundi kupanga mikakati yao walivyokuwa wakifanya. Kwa sasa mawasiliano ni kupitia simu na mitandao ya kijamii. Kinachowapa wakati mgumu ni kuwasiliana na wapigakura,” asema Bi Sambu.
Wanasiasa wengine walioonekana mitandaoni wakiendeleza shughuli zao japo kwa njia moja au nyingine wakijitangaza ni Naibu wa Rais William Ruto aliyesawiriwa kwake Sugoi akipalilia kabichi, japo baadaye alikanusha, na mbunge wa Dagoretti Kaskazini, Simba Arati aliyechapisha bango likieleza wananchi jinsi ya kujizuia na virusi hatari vya corona.