Dondoo

Polo aliyekojoa kitandani ajuta

April 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na TOBBIE WEKESA

BUSIADA, BUSIA

MWANADADA wa hapa aliwafanya wakazi kucheka kwa kumlazimisha mumewe mlevi kuanika malazi aliyolowesha kwa mkojo.

Kulingana na mwanamke huyo, mumewe alikuwa na tabia ya kukojoa kitandani mara kwa mara.

Duru zinaarifu kwamba jioni moja baada ya kulewa, polo alitangulia kitandani.

Inasemekana mkewe aliamua kupitisha wakati kwa kujishughulisha na kazi za jikoni huku akisubiri jamaa apate usingizi.

Baada ya saa mbili kupita alielekea kitandani na hakuamini alichokiona.

“Umekuwa ukisema ni mimi huwa ninakojoa kitandani. Huu mkojo nani amekojoa,” kipusa alifoka.

Jamaa alishtuka kutoka usingizini. “Nani amekwambia kuwa huu ni mkojo. Haya ni maji,” polo alijitetea.

Duru zinasema kipusa aliinama na kunusa ili kubaini madai ya polo.

“Maji gani yananuka hivi. Una ujinga sana. Nimekuvumilia kwa muda mrefu,” kipusa alimkaripia polo.

Polo alibaki ameduwaa asijue la kufanya naye kipusa akaamua kulala kwenye kiti akisubiri asubuhi ifike.

Habari zilizotufikia zinasema mwanadada hakungoja jua lichomoze.

“Huendi popote kabla hujaanika malazi,” demu alimkaripia jamaa.

“Acha kujifanya hapa. Mzee mzima kama wewe unaosha malazi kwa mkojo moto hivi,” alimkaripia.

Majirani walibaki vinywa wazi. Wenye kucheka walicheka.

“Tangu niolewe na huyu jamaa hakuna siku nimekosa kuanika malazi. Nikimuuliza kwa nini hukojoa kitandani huwa ankunitusu,” mwanadada alidai.

Duru zinasema jamaa hakuwa na jingine ila kustahimili shinikizo na aibu na kuamua kuanika malazi huku kila mtu akimtazama.

“Ukiendelea kukojoa utakuwa ukianika malazi. Na malazi yakinuka walahi utapeleka mtoni kuosha,” alimuonya polo.