• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
Gura Arsenal na utafute klabu kubwa inayokufaa, Aubameyang ashauriwa na Gabon

Gura Arsenal na utafute klabu kubwa inayokufaa, Aubameyang ashauriwa na Gabon

Na CHRIS ADUNGO

RAIS wa Shirikisho la Soka la Gabon, Pierre Alain Mounguengui, amemtaka nahodha na mvamizi matata wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang kujiunga na kikosi cha haiba kubwa zaidi kitakachofanikisha mengi ya matamanio yake kitaaluma.

Aubameyang ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Gabon, alifunga jumla ya mabao 22 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu uliopita na kutawazwa mfungaji bora wa kivumbi hicho kwa pamoja na Sadio Mane na Mohamed Salah wa Liverpool. Mane na Salah pia ni wachezaji wa timu za taifa za Senegal na Misri mtawalia.

Mkataba wa sasa kati ya Arsenal na Aubameyang, 30, unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

“Kwa sasa ni tegemeo kubwa kambini mwa Arsenal, na hajashinda taji lolote katika kikosi hicho. Hivyo, hakuna tofauti kubwa kati yake na mchezaji yeyote mwingine aliyefeli kitaaluma,” akatanguliza Mounguengui.

“Japo sitaki kueleweka kwamba Arsenal hawana maazimio yoyote, mshawasha wao wa kutaka kufaulu si wa juu zaidi ikilinganishwa na vikosi vingine katika soka ya bara Ulaya,” akaongeza kinara huyo.

Mwishoni mwa mwezi jana, kocha Mikel Arteta wa Arsenal alisisitiza kwamba atafanya lolote lililopo chini ya uwezo wake kuhakikisha kwamba Aubameyang anarefusha kandarasi yake kambini mwa kikosi hicho.

Hadi kusitishwa kwa kipute cha EPL msimu huu kutokana na mlipuko wa virusi vya corona, Aubameyang alikuwa amewafungia Arsenal jumla ya mabao 20 katika mashindano yote.

Huu ni ufanisi ambao umemfanya kuwa kivutio kikubwa kambini mwa Barcelona (Uhispania) na Inter Milan (Italia) ambao kwa sasa wapo radhi kumshawishi kujiunga nao kwa ahadi ya mshahara mnono zaidi wa hadi Sh56 milioni kwa wiki.

“Iwapo Aubameyang ataingia katika sajili rasmi ya kikosi kilicho na malengo makubwa zaidi, naye aendelee kutawaliwa na kiu ya ushindi, basi atakuwa kielelezo chema kabisa kwa chipukizi wengi ndani na nje ya Gabon,” akasema Mounguengui.

“Kwa sasa ni kipenzi cha wakazi wengi wa Gabon, hasa kwa vijana chipukizi wanaotazamia kufikia ngazi ya mafanikio yake. Katika kiwango chake, anastahili skustaafu akivalia jezi za klabu kubwa zaidi, ajinyakulie mataji ya haiba na ashindie Gabon ubingwa wa Kombe la Afrika (AFCON),” akaongeza.

Tangu ajiunge na Arsenal kwa kima cha Sh7.8 bilioni kutoka Borussia Dortmund mnamo Januari 2018, Aubameyang ameshuhudia kikosi chake kikibanduliwa kwenye fainali za Europa League na Carabao Cup; na bado hajanyanyua taji lolote ugani Emirates.

You can share this post!

Soko jipya la Limuru lafunguliwa

Wanawake 2 wafariki kwa mkanyagano wa chakula cha msaada...

adminleo