Michezo

Tyson Fury kupigana na Deontay Wilder tena

April 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CHRIS ADUNGO

MWANAMASUMBWI Tyson Fury ambaye ni mshikilizi wa taji la WBC la uzani wa ‘heavy’ – la pekee ambalo Mwingireza Anthony Joshua hana – ameratibiwa kuchapana na Deontay Wilder wa Amerika kwa mara ya tatu mnamo Oktoba 2020. Haya ni kwa mujibu wa promota wa Fury, Frank Warren.

Fury alimdengua Wilder kwa njia ya ‘Knock-Out’ katika raundi ya saba jijini Las Vegas, Amerika mnamo Februari mwaka huu. Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Fury kumzidi maarifa Wilder baada ya wawili hao kuambulia sare mnamo 2018 jijini Los Angeles.

Kwingineko, Joshua, hataweza kutetea mataji yake ya kimataifa ya IBF, WBA, WBO na IBO katika uzani wa ‘heavy’ baada ya pigano dhidi ya Kubrat Pulev wa Bulgaria kuahirishwa.

Wawili hao walikuwa wameratibiwa kuchapana katika uwanja wa Tottenham Hotspur jijini London, Uingereza mnamo Juni 20, 2020.

Kwa mujibu wa Matchroom Boxing ambao ni mapromota wa Joshua, tarehe mpya ya kuandaliwa kwa ndondi hizo itatolewa hivi karibuni, japo watajitahidi kuhakikisha kwamba pigano hilo bado linaandaliwa ugani Tottenham.

Joshua, 30, hajashiriki pigano lolote tangu Disemba 2019 alipomzidi maarifa Andy Ruiz Jr kwa wingi wa alama nchini Saudi Arabia. Mchapano huo uliompa Joshua jukwaa la kurejesha ufalme aliokuwa amepokonywa hapo awali na mwanamasumbwi huyo mzawa wa Amerika na raia wa Mexico jijini New York mnamo Juni mwaka jana.

Pulev, 38, atakuwa akiwania fursa ya kutwaa taji la IBF kutoka kwa Joshua. Awali, wawili hao walikuwa wamepangwa kumenyana mnamo Oktoba 2017 uwanjani Cardiff Principality, Uingereza. Hata hivyo, Pulev alijiondoa katika dakika za mwisho baada ya kupata jeraha baya la bega.

Michuano yote iliyokuwa imeratibiwa na Bodi ya Ndondi ya Uingereza hadi mwisho wa Mei 2020 imefutiliwa mbali kutokana na virusi vya corona vinavyozidi kutikisa ulimwengu mzima.

Eddie Hearn ambaye ni promota wa Pulev amedokeza uwezekano wa pigano kati ya wakala wake na Joshua kufanyika Julai baada ya suitafahamu kuibuka kuhusu wakati ambao kikosi cha Totteham Hotspur kitakamilisha mechi za nyumbani katika kivumbi cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambacho sasa kimeahirishwa kwa muda usiojulikana.