Michezo

Gitothua wapanga kukuza vipaji vya mabinti na wavulana

April 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

TIMU za michezo mbalimbali huanzishwa kwa malengo tofauti ikiwamo kunoa makucha ya wachezaji wazo wakipania kupaisha ujuzi wao na kutinga kiwango cha kushiriki mashindano ya kimataifa miaka ijayo.

Miaka ya sasa spoti imeibuka kitega uchumi kwa wengi duniani, wanaume kwa wanawake, anasema meneja wa timu ya wanawake ya Gitothua Starlets, Victor Mwasaru. Anasema kituo hicho kwa sasa kimeibuka kuwa akademia ambapo wanalenga kukuza wachezaji wengi tu wasichana na wavulana waliotunukiwa kipaji cha kugaragaza gozi maeneo hayo.

Meneja huyo anasema licha ya janga la korona kusitisha shughuli za michezo nchini bado hawajayeyusha malengo yao kushiriki kipute cha Aberdare Regional League (ARL) baada ya kukosa ufadhili kucheza Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza.

”Sina shaka kutaja kuwa kituo chetu kinazidi kupanua mabawa maana tayari tumeanzisha timu ya wavulana waliokuwa wakija kutazama wasichana wakicheza,” anasema na kuongeza kuwa wanatoa mwito kwa wahisani wajitokeze ili kuwashika mkono kutimiza azimio lao.

Meneja huyo anashikilia kuwa wanalenga kuendelea kushirikisha wasichana katika mchezo wa soka hasa wanafunzi ili kupata ufadhili ya elimu katika shule za upili. Anadokeza kuwa wasichana wengi wametoka familia maskini ambazo haziwezi kugharamia elimu ya sekondari.

Chini ya mwavuli wa Gitothua Starlets wasichana sita waliofanya mtihani wa darasa la nane miaka miwili iliyopita wana tabasamu. Kati yao wakiwa Risper Wanjiku, Judy Wambui na Esther Anupi waliofanikiwa kupata udhamini wa elimu ya sekondari katika shule ya Migori Education Centre. Wengine walijiunga na shule ya Wiyeta Girls na Madira Girls.

Ikiwa ni chini ya miaka miwili kituo hicho kimefanikiwa kusaidia wavulana wanane kupata ufadhili kujiunga na shule za sekondari ambapo wawili wao walijiunga na shule ya Nduru Boys katika Kaunti ya Kisii.

Makocha ya kikosi hicho, Michael Mwamburi na mwenzake, John Baraka wanaamini wana uwezo wa kufanya vizuri katika soka la wasichana. Kocha John Baraka anasema “Timu ya wavulana kwa wasiozidi umri wa miaka 15 imefanikiwa kushiriki mashindano ya kuwania taji la Joe Kadenge ambayo huandaliwa kila mwaka jijini Nairobi. Tulifanikiwa kumaliza katika nafasi ya nne. Anadokeza kuwa matokeo hayo yalidhirisha wazi kuwa chipukizi hao wana talanta ya kufanya vizuri katika soka.

Kufuatia mkurupuko wa virusi vya korona meneja huyo anasema wanalenga kutoa msaada wa chakula kwa familia za wachezaji wao hivi karibuni. Kadhalika anadokeza kuwa wanawazia pia kutoa kwa familia zilizo majirani wao katika mtaa huo wa Gitothua.