• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
Watford, Southampton na West Ham zakata wachezaji mishahara

Watford, Southampton na West Ham zakata wachezaji mishahara

Na CHRIS ADUNGO

WATFORD wanatarajiwa kuwa kikosi cha tatu baada ya Southampton na West Ham katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kushawishi wachezaji wao kukubali kunyofolewa sehemu ya mishahara yao kutokana na janga la corona.

Mapema mwezi huu, Southampton na West Ham walithibitisha kwamba masogora wao wamekubali kukatwa posho katika mojawapo ya kufanikisha juhudi za kukabiliana vilivyo na mlipuko wa corona.

Wanasoka wa Arsenal wanatarajiwa pia kukubali kupunguziwa asilimia 12.5 ya mishahara yao huku Chelsea wakifichua azma ya kunyofoa asilimia 10 kutoka kwa ujira wa kila mwezi wa wachezaji wao.

Mbali na wachezaji, maamuzi ya Watford yatawaathiri pia wasimamizi wakuu wa kikosi hicho na kocha Nigel Pearson.

Mazungumzo ya kufanikisha mpango huo wa Watford ulianzishwa Jumapili huku baadhi ya wachezaji wakipendekeza asilimia 30 ya mishahara yao kukatwa.

West Ham ilikuwa klabu ya pili baada ya Southampton kutangaza kwamba itanyofoa asilimia 20 ya mshahara wa wachezaji wake. Mkufunzi David Moyes, Naibu Mwenyekiti Karren Brady na Mkurugenzi wa Fedha Andy Mollet kwa sasa wanapunguziwa mshahara kwa asilimia 30.

Aidha, David Sullivan na David Gold ambao ni wenyeviti wa West Ham wameapa kushirikiana na wadau wengine ili kuongeza takriban Sh4.2 bilioni katika hazina ya klabu hiyo.

Kwa mujibu wa West Ham, hatua yao hiyo itawawezesha vibarua wao wote kuhifadhi kazi zao huku wakidumishwa kwa asilimia 100 ya mishahara.

Baadhi ya klabu za EPL zimetaka wachezaji wao kukubali kupunguziwa mshahara kwa hadi asilimia 30 ili kumudu gharama ya matumizi ya fedha na kuwapa wahudumu wao wengine wasiokuwa wachezaji fursa za kuhifadhi kazi zao mbalimbali.

Hii ni baada ya vinara wa soka ya Uingereza kufichua ugumu wa kurejelewa kwa kipute cha EPL mnamo Mei, 2020 kama ilivyoratibiwa awali; na badala yake kusisitiza kuwa kinyang’anyiro hicho kitaanza upya pindi virusi vya homa kali ya corona vitakapodhibitiwa vilivyo na kukamilika chini ya siku 56 kabla ya Juni 30, 2020.

Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) limetaka pia Sh17.5 bilioni kutolewa kwenye bajeti ya EPL msimu huu na fedha hizo kupokezwa klabu mbalimbali za madaraja ya chini na Ligi ya Kitaifa. Sh2.8 bilioni zaidi kutoka bajeti ya EPL zitatolewa kwa minajili ya vifaa vya afya katika hospitali mbalimbali nchini Uingereza.

You can share this post!

Wachezaji wa Roma wakubali kujinyima mshahara kwa miezi 4...

Guardiola asajili beki chipukizi wa Peru

adminleo