• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 8:55 AM
Sharp Boys wajiandaa kwa msimu ujao

Sharp Boys wajiandaa kwa msimu ujao

Na JOHN KIMWERE

SHARP Boys kwa mara ya kwanza imeshinda taji la Top 8 kwa timu zilizoshiriki Ligi ya KYSD msimu wa 2019/2020 kwa wasiozidi umri wa miaka 14.

Kando na ubingwa huo pia iliwahi kubeba ubingwa wa ligi hiyo mara moja tangu ianzishwe mwaka 2000. Sharp Boys ambayo hunolewa na kocha, Boniface Kyalo kwenye kampeni za ligi ilimaliza ya nne kwa alama 58, moja mbele ya Lemans F.A.

Chipukizi hao chini ya nahodha, Wyne Orata na msaidizi wake, David Mwangi walifunga Tico Raiders mabao 3-2 katika fainali iliyoshuhudia ushindani wa kufa mtu.

Sharp Boys ilishinda wapinzani wao kupitia mipigo ya penalti baada ya kutoka sare tasa katika muda wa kawaida. Waliofungia Sharp Boys walikuwa Ramadhan Mohammed, Victor Mugambi na Victor Aguya.

Sharp Boys ilionyesha ukakamavu wake iliponyuka waliokuwa mabingwa watetezi Kinyago United kwa mabao 2-0 kwenye nusu fainali ya kwanza. Kwenye nusu fainali ya pili, Tico Raiders ilivuna bao 1-0 dhidi ya Lemans F.A.

Naibu kocha, Peter Maundu anashukuru kikosi hicho kwa kazi njema kiliofanya licha ya kutotwaa ubingwa wa ligi.

Kikosi cha Sharp Boys

”Kusema kweli chipukizi wangu walifanya kazi ya kuvutia kwenye kampeni za msimu uliyokamilka. Kubeba taji la Top 8 haikuwa kazi rahisi hasa kushinda Kinyago United ambayo imekuwa ikishinda taji hilo karibu kila mwaka” alisema.

Kocha mkuu aliongeza kuwa anajivunia kikosi chake kimekaa vizuri pia anatarajia kitakuwa imara kwenye kampeni za msimu ujao.

”Tatizo kuu kwa muda huu janga la ugonjwa wa COVID-19 limezima shughuli zetu maana hatushiriki mazoezi kabisa,” alisema Kyalo.

Kocha huyo aliongeza kuwa watakosa huduma za wachezaji wanne ambao watapanda ngazi kujiunga na timu ya wasiozidi umri wa miaka 16.

”Sharp Boys hutumia soka kuwaleta pamoja vijana chipukizi hasa kuwasadia kupiga chenga matendo maovu mitaani ikiwamo matumizi ya mihadarati kati ya mengine,” alisema na kuongeza kuwa juhudi zao zimesaidia wengi kupiga hatua kimasomo.

Vijana tisa wachezaji wake tayari ni wanasoma vyuo vikuu mbali mbali pia zaidi ya wenzao 20 wanasoma Shule za sekondari tofauti nchini.

Kadhalika anasema Melvin Kamau ambaye ni askari wa magereza alipitia mikononi mwake. Sharp Boys inajivunia kunoa makucha ya wachezaji wengi tu ambao huchezea vikosi tofauti ambavyo hushiriki mechi za Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).

Orodha yao inajumuisha: Tryon Omondi (Posta Rangers Youth), Bravin Omondi (Tusker Youth), Christopher Muriithi (Nunguni FC ya Machakos), Hussein Maina, William Okwasumi na Sudeis Hussein wote Uprising FC ambayo hushiriki Ligi ya Taifa daraja la Pili.

Sharp Boys inajumuisha chipukizi hawa: Mohamed Ramadhan, David Mwangi, Wayne Orata (nahodha), Edward Njuguna, Carlos Odingo, Victor Mugambi, Simon Nzivo, Steve Mugambi, Eric Mutiso, Victor Aguya, Ayale Muktar, Joseph Orenga, Kevin Omondi na Hillary Busenei.

You can share this post!

Polisi waliokubalia watu wenye corona kuingia Homa Bay...

MR BEE: Mmliki wa studio ya kunoa vipaji vya chipukizi

adminleo