Kenya yamwomboleza bondia Douglas Maina
Na GEOFFREY ANENE
KENYA inaomboleza kifo cha mshindi wa medali za shaba za Michezo ya Jumuiya ya Madola (Canada) na African Games (Algeria) mwaka 1978, Douglas Maina.
Maina, ambaye alipata medali hizo kwenye uzani wa kilo 52-53 (bantam), aliaga dunia nyumbani kwake jijini Nairobi usiku wa kuamkia Aprili 23, 2020.
Taarifa kutoka kwa familia yake zimesema Alhamisi alikuwa mgonjwa kwa muda mrefu.
Baadhi ya Wakenya, ambao tayari wametuma rambirambi zao kwa familia yake ni Kamati ya Olimpiki Nchini (NOC-Kenya) na Mratibu wa Kitaifa wa Mashujaa Wanaume na Wanawake michezoni Rose Tata-Muya.
Maina alikuwa katika kikosi cha wanamasumbwi waliozolea Kenya medali saba kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola mjini Edmonton, Canada mwaka 1978. Mabondia wengine walioshindia Kenya medali ni Stephen Muchoki (uzani wa Light Fly) na Michael Irungu (uzani wa Fly), ambao walinyakua dhahabu, nao Patrick Waweru (uzani wa Light) na Abdulrahman Athuman (uzani wa Light Middle) wakazoa nishani za fedha. Michael Mawangi (uzani wa Light Welter) na Edward Thande (uzani wa Light Heavy) walivuna nishani za shaba.