Kivumbi cha London Marathon kutifuliwa na wanariadha wa haiba kubwa pekee
Na CHRIS ADUNGO
MBIO za zilizoahirishwa za London Marathon huenda zikawashirikisha wanariadha wazoefu na wa haiba kubwa zaidi pekee mwaka huu 2020.
Haya ni kwa mujibu wa mkurugenzi wa mbio hizo, Hugh Brasher.
Brasher amesema kwamba hilo ni mojawapo kati ya mapendekezo 10 ambayo yamekuwa yakibadilika mara kwa mara kuhusiana na mbio hizo ambazo huenda zikaahirishwa hata zaidi.
Kivumbi cha London Marathon kilichotazamiwa kufanyika Jumapili ya Aprili 26, 2020 kiliratibiwa upya hadi Oktoba 4, 2020 kwa sababu ya mlipuko wa virusi vya corona.
Takriban wanariadha 43,000 walishiriki mbio za London Marathon mnamo 2019.
Mkenya Eliud Kipchoge na Kenenisa Bekele wa Ethiopia wanatarajiwa kunogesha kivumbi cha mwaka huu kwa upande wa wanaume.
“Tunatazamia kuwaalika tena Kipchoge na Bekele kushiriki mbio hizi tulizozihamishia Oktoba 2020 japo hatuna mwao kabisa kuhusu kitakachofanyika kati ya sasa na wakati huo,” akatanguliza Brasher.
“Inatulazimu kuitathmini kila hali kwa upana wake huku tukizaingatia usalama wa mamilioni ya mashabiki, wadau wengine na maafisa wa afya,” akaongeza kinara huyo akifichua uwezekano wa kuigwa kwa namna ambayo Tokyo Marathon iliendeshwa mwezi uliopita.
Mbio za Tokyo Marathon nchini Japan zilijumuisha wanariadha wachache zaidi wa haiba kubwa huku mashabiki wakizuiliwa kabisa kujitokeza barabarani kushabikia na kutilia shime washiriki wa kivumbi hicho.
Mbali na London Marathon, kivumbi kingine cha haiba kubwa ambacho kimeahirishwa mwaka 2020 ni Berlin Marathon kilichokuwa kiandaliwe mnamo Septemba 27, 2020.
Kusitishwa kwa mbio hizo kulitokana na hatua ya serikali ya Ujerumani kupiga marufuku mikusanyiko yote ya umma hadi Oktoba 24.
Brasher amesema kwamba anashauriana na wakurugenzi wengine wa marathon zote kuu nyinginezo duniani na maamuzi yatakayotokana na mashauriano hayo yatafichuliwa wakati wowote wiki ijayo.