Habari

Rais avunja itifaki

April 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyattta alivunja itifaki Jumamosi alipowaruhusu magavana Ali Hassan Joho (Mombasa), Amason Kingi (Kilifi) na Salim Mvurya (Kwale) kuhutubu kutoka kwa jukwaa la Rais (Presidential Podium) katika Ikulu ya Nairobi.

Kiongozi wa taifa alizima jaribio la mhudumu mmoja wa Ikulu la kumpa Joho kinasa sauti – maikrofoni – tofauti na kuamuru kuwa gavana huyo aruhusiwe kuhutubu kupitia jukwaa la urais.

Magavana Kingi na Mvurya pia walipewa nafasi iyo hiyo, ya kutumia chombo hicho cha hadhi, kuelezea changamoto ambazo kaunti zao zinapitia kutokana na janga la Covid-19.

Ni utaratibu wa kawaida kwamba baada ya Rais kuhutubia taifa, jukwaa lake huondolewa na wanenaji wengine hutumia maikrofoni tofauti.

Ni marais na viongozi wa nchi za kigeni pekee ambao huruhusiwa kutumia jukwaa hilo la Rais.

Gavana Joho aliwashauri Wakenya kuwajibika na kuzingatia kanuni zote zilizowekwa na Wizara ya Afya kwa ajili ya kupunguza kuenea kwa virusi vya corona.

“Kuna yale ambayo serikali yako itafanya na itaendelea kufanya kuendeleza vita dhidi ya janga hili. Lakini ukweli ni kwamba ukichunguza katika mataifa kadha ulimwenguni utagundua asilimia 90 ya wajibu huu ni wenu kama wananchi,” akaeleza.

Aliongeza kuwa wananchi wanaweza kuzuia kuambukizwa ikiwa watafuata maagizo ya serikali lakini akasikitika kuwa baadhi ya wakazi wa kaunti yake hawazingatii masharti hayo na ndio maana virusi hivyo vinasambaa huko kwa kasi mno.

“Huenda watu wetu wanahitaji kuwekewa masharti zaidi makali. Wale watakaoathiriwa zaidi ni wananchi; na ni wao pia walio na suluhu ikiwa watazingatia maagizo ya wataalamu.” akaongeza.

Akiunga mkono kauli za Joho gavana Mvurya alisema kuwa janga la corona limeathiri pakubwa sekta ya utalii ambayo ndio chanzo cha mapato kwa eneo la Pwani.

Gavana Kingi pia alikariri wajibu mkubwa wa wananchi katika vita dhidi ya janga la corona, akihimiza ushirikiano baina ya serikali kuu na zile za kaunti katika vita dhidi ya janga hili.

Gavana Sonko hakuwepo katika Ikulu ya Nairobi licha ya kwamba Kaunti ya Nairobi ni mojawapo kati ya zile zilizoathirika zaidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Hali hiyo ndio ilisababisha serikali kuweka amri ya watu kutoingia na kutotoka kaunti hizo nne na wiki jana ikaongeza Mandera katika orodha hiyo.

Kwa hakika kati ya wagonjwa 343 wa Covid-19 ambao wamethibitishwa nchini Kenya kufikia Jumamosi, 230 wanatoka Nairobi.