Hakuna nafuu licha ya bei ya mafuta kushuka

Na EDWIN OKOTH

HAKUNA matumaini kwa Wakenya kunufaika na bei ya chini ya mafuta iliyotangazwa mwezi huu wa Aprili.

Mamlaka ya kudhibiti bei ya kawi nchini (EPRA) ilitangaza bei ya chini zaidi ya mafuta takribani wiki mbili zilizopita ambapo kwa mara ya kwanza tangu 2010, petroli aina ya supa iliuzwa kwa bei ya chini kuliko diseli.

Na licha ya kushuka kwa bei hiyo, watengenezaji wa bidhaa ambao hutumia gharama ya uchukuzi kukadiria bei ya bidhaa zao hawajapunguza bei za bidhaa.

Wamiliki wa matatu wanasema kwamba hata kushuka kwa bei ya diseli kwa Sh20 hakuwezi kuchangia nauli kushuka ikizingatiwa kuwa biashara zimeathiriwa vibaya na janga la corona

Mwenyekiti wa chama cha wamiliki wa matatu, Bw Simon Kimutai aliambia Taifa Jumapili kwamba mbali na kuathiriwa na janga la corona, biashara ya matatu huwa haina faida na kwa hivyo ni vigumu nauli kupunguzwa pale bei ya mafuta inaposhuka.

“Tunapata hasara kubwa sana sasa kwa sababu hakuna watu wanaosafiri. Hatuwezi hata kumudu gharama ya huduma na ikiwa tunatumia lita 29 kubeba watu 60, mapato kutoka kwa mafuta ni Sh200, tutagawa vipi hiyo kwa watu 60? Mafuta si gharama ya pekee tuliyonayo; kuna bima, kutunza gari ambalo thamani yake hupungua kila siku. Ni kawaida matatu kuongeza nauli watu wengi wanaposafiri, sawa tu na jinsi bei ya chakula inavyopanda msimu wa Krismasi,” alisema Bw Kimutai.

Wadau wengi hawaamini kuwa abiria watanufaika na kushuka kwa bei ya mafuta.

Katibu Mkuu wa shirikisho la watumiaji bidhaa nchini (Cofek), Bw Stephen Mutoro, alisema Wakenya wanateseka kwa sababu serikali haijaweka sheria thabiti, maafisa fisadi wa serikali na mbinu chafu za wafanyabiashara.

Bw Mutoro anaamini kwamba kuna haja kuwa na sera thabiti ya kuhakikisha kuwa Wakenya wanafaidika kila wakati gharama ya utengenezaji bidhaa inaposhuka.

“Kukosa kupunguzia Wakenya gharama hakuna uhusiano na masuala ya uchumi, ni kukosa kuadhibiwa na kuwepo kwa mapengo mengi katika usimamizi. Epra, inayodaiwa kudhibiti bei haiwezi hata kueleza jinsi kushuka kwa bei kunavyoathiri masoko. Hakuna shirika la serikali linalofuatilia ili kuhakikisha bei zilizopendekezwa zinatekelezwa. Hakuna shirika linalohusika na usimamizi, lililo na mwaklishi wa watumiaji bidhaa wala hakuna anayeshughulika kujua jinsi Wakenya wananufaika,” alisema Bw Mutoro.

Hali sawa na hiyo hushuhudiwa serikali inapowapa wafanyabiashara vibali vya kuagiza bidhaa kutoka nje bila kulipa ushuru ambapo wafanyabiashara walafi, maafisa fisadi wa serikali na mawakala hupata faida kubwa kutoka kwa bidhaa ambazo hawalipii ushuru na ambazo hunuiwa kupatia umma afueni wakati wa hali ngumu kiuchumi.

Uagizaji wa mbolea ya bei nafuu mwaka wa 2018 ulivurugwa na ununuzi wa mbolea feki, nazo siasa zilivuruga uagizaji wa sukari mwaka wa 2017.

Serikali ililazimika kutisha kuwafunga jela wafanyabiashara ili wapunguze bei ya unga wa mahindi baada ya kampuni kuuziwa mahindi ya bei nafuu.

Habari zinazohusiana na hii