Kibera Black Stars waweka malengo mapya

Na CHRIS ADUNGO

KIBERA Black Stars wameapa kufuzu kwa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) katika kipindi cha misimu miwili ijayo.

Kikosi hicho kinachojidhamini kwa sasa kinashikilia nafasi ya 16 kwenye msimamo wa jedwali la Ligi ya Kitaifa ya NSL kwa alama 21.

Kwa mujibu wa Daniel Magara ambaye ni Katibu Mkuu wa klabu hiyo, kinachowaaminisha zaidi kwamba Black Stars watapanda daraja chini ya kipindi kifupi kijacho ni ukubwa wa viwango vya ushindani na msukumu wa ndani kwa ndani miongoni mwa wachezaji wao.

“Nafasi yetu jedwalini haisemi hadithi nzima kuhusu upekee wa uwezo wa Black Stars. Ilivyo, vijana wetu wana ari na kiu kubwa ya kutamba katika NSL na kupanda ngazi kushiriki kivumbi cha KPL chini ya kipindi cha miaka miwili ijayo,” akasema Magara akishikilia kwamba maazimio yao kwa sasa ni kukamilisha kampeni za msimu huu ndani ya mduara wa 10-bora kisha kutinga sita-bora muhula ujao.

“Kukamilisha kampeni za muhula ujao miongoni mwa vikosi sita vya kwanza kileleni mwa jedwali kutatupa mshawasha zaidi kadri tunavyolenga kunogesha kipute cha KPL kufikia 2022.”

Kwa mujibu wa Magara, Black Stars wamekuwa na panda-shuka tele msimu huu kutokana na uchechefu wa fedha uliokuwa kiini cha kubanduka kwa nyota Nicholas Omondi na Julius Masaba walioyoyomea Gor Mahia na Kariobangi Sharks mtawalia mnamo Januari 2020.

Mbali na hao, wachezaji wengine waliokuwa wa haiba kubwa kambini mwa Black Stars waliingia katika sajili rasmi za Posta Rangers na Coast Stima.

“Wachezaji hawa waliokuwa tegemeo kubwa la Black Stars waliacha pengo kubwa ambalo limetuchukua muda mrefu kuziba,” akaongeza Magara kwa kufichua kwamba wengi wa wachezaji wao hutokea ni wanafunzi waliokamilisha masomo yao ya shule za sekondari hivi majuzi kutoka maeneo ya Kibera, Dagoretti, Kawangware na Satellite.

Nafasi bora zaidi ambayo imewahi kushikiliwa na Black Stars katika kipute cha NSL ni ya tano misimu mitano iliyopita. Mojawapo ya mikakati yao ni kujishughulisha vilivyo katika soko la uhamisho na kujitwalia huduma za wachezaji wa haiba zaidi kivumbi cha NSL kitakaporejelewa baada ya virusi vya corona kudhibitiwa vilivyo.

Miongoni mwa wachezaji ambao kwa sasa ni mhimili kubwa kambini mwa Black Stars ni Eric Odhiambo, Peter Onduso, Daniel Omwanda na Hillary Omondi ambao Magara amesema wanabeba matumaini ya mafanikio ya kikosi mabegani pao.

Hadi kusimamishwa kwa gozi la NSL, Nairobi City Stars walikuwa wamejizolea alama 64 zinazowaweka kileleni mwa jedwali. Bidco United wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 54, mbili zaidi kuliko Vihiga United.

Habari zinazohusiana na hii