• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
BODABODA: Sekta inayopaswa kudhibitiwa kabla maji kuzidi unga

BODABODA: Sekta inayopaswa kudhibitiwa kabla maji kuzidi unga

Na SAMMY WAWERU

BODABODA ni mojawapo ya sekta zilizojiri wengi kupitia mikakati ya urahisishaji utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.

Sekta hiyo inasifiwa kwa kubuni maelfu ya nafasi za ajira kwa vijana waendeshaji pikipiki.

Isitoshe, sekta hiyo imesaidia kurahisisha shughuli za usafiri na uchukuzi, hususan maeneo yasiyoingilika magari.

Kimsingi, huduma za bodaboda zinategemewa na mamilioni ya watu nchini.

Licha ya manufaa yake, imetajwa kuhusishwa na visa mbalimbali vya uhalifu. Si kisa kimoja, viwili au vitatu, pikipiki zimeripotiwa kutekeleza uhalifu maeneo tofauti nchini.

Pia, wahudumu wa bodaboda wanalaumiwa kuzua vita, uvamizi na hata mauaji, kwa wanaoonekana kutofautiana nao barabarani. Ni sekta ambayo wengi wa wahudumu hawatii kanuni na sheria za trafiki hasa mijini.

Mwaka 2019 Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i akifufua sheria za ‘Michuki’, aliamuru wahudumu wa bodaboda kuheshimu sheria za trafiki.

Aidha, waziri huyo aliwapa muda kupata mafunzo ya uendeshaji bodaboda ikiwa ni pamoja na leseni, hatua ambayo kufikia sasa imeonekana kufifia.

Kando na kuhitimu mafunzo ya udereva na kuwa na leseni, pikipiki zinapaswa kuwa na bima, wahudumu wawe na mavazi maalum na barakoa mbili.

Machi 2020 Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitaja sekta hiyo kama mojawapo ya vichocheo vya ueneaji wa Covid-19, ugonjwa ambao umesababisha vifo vya watu kadhaa nchini na mamia kuambukizwa.

Akiendelea kuhimiza Wakenya kujikinga dhidi ya virusi hivyo, Bw Kagwe alitoa kanuni mpya kwa waendeshaji bodaboda kuzuia maambukizi kati yao na wateja.

Waziri aidha aliwataka wahudumu hao kubeba abiria mmoja, akitaka kila mmoja kuvaa barakoa.

“Dereva na abiria wake wavae barakoa,” Bw Kagwe aliamuru.

Pia, aliahidi kuwa serikali itasambaza barakoa zaidi katika kila kaunti, ili kuzuia maambukizi zaidi ya Covid – 19 kupitia usafiri wa bodaboda.

Waziri alionya kuwa watakaokaidi kanuni hiyo watalazimishwa na maafisa wa polisi.

Kanuni alizotaja ni miongoni mwa sheria za trafiki wanazopaswa kuafikia wahudumu hao. Ili kuchukua tahadhari dhidi ya Covid-19, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe aliwakumbusha tu.

Kwa hakika ni sekta iliyosheheni ubaradhuli, tabia ya kutokuwa na adabu au heshima kwa watu. Si ajabu kuona mhudumu wa bodaboda, anapotofautiana na dereva wa gari, anashawishi wenzake wanaishia ‘kumwadhibu’ na hata kuteketeza gari lake.

Visa vingi vya ajali nchini pia vinahusishwa na wanabodaboda, kwa sababu ya kupuuza sheria za trafiki. Hata ingawa kuna wenye heshima, wengi wao ni mabaradhuli wanaokaidi kanuni za trafiki na kuona wamepiku sheria.

La kushangaza, asilimia kubwa kati yao hawajapitia mafunzo ya udereva, ambapo hujifunza namna ya kuendesha bodaboda kule mashinani, siku moja, ya pili, na ya tatu anaingia barabarani.

Mhudumu wa aina hiyo ataelewa vipi bayana kanuni na sheria za trafiki?

Ni sekta inayoonekana kufumbiwa macho na serikali.

Kuzuia maambukizi ya Covid-19 kwao na kwa wateja, isiwe ndiyo sababu ya kuwataka kuvalia barakoa.

Sheria hiyo ni miongoni mwa wanazopaswa kutii kila wakati wakiwa barabarani. Inapaswa kudhibitiwa kabla maji kuzidi unga.

You can share this post!

Waathiriwa wa mafuriko wasaidiwa

Bei ya unga wa mahindi yapanda

adminleo