Habari

Serikali yatangaza kanuni mpya za kufungua mikahawa

April 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na VALENTINE OBARA

SERIKALI hatimaye imetangaza kanuni ambazo zitatumiwa kuruhusu mikahawa kuendeleza biashara zao bila kuweka wateja na wahudumu katika hatari ya kueneza virusi vya corona.

Kanuni hizo zilitangazwa Jumatatu na Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe, huku idadi ya waliopona ugonjwa wa Covid-19 ikipanda hadi watu 114.

Kufikia Jumatatu, idadi ya watu walioambukizwa pia iliongezeka hadi watu 363 baada ya watu wanane kupatikana wameambukizwa.

Wanatoka kaunti za Mombasa, Kwale na Nairobi.

Mikahawa mingi mijini ilifungwa wakati serikali iliposema watu wataruhusiwa tu kununua chakula cha kubeba ili kuzuia ueneaji wa virusi vya corona.

Katika masharti mapya, Bw Kagwe alisema ni lazima kila mhudumu athibitishwe hajaambukizwa corona kabla mkahawa ukubaliwe kuendelea na kazi.

Watu hawatakubaliwa kuingia wengi kwa wakati mmoja, na watakaoingia watahitajika kukaa mita moja unusu kutoka kwa wengine kila upande. Hakuna atakayeruhusiwa kutembeatembea ndani ya mkahawa isipokuwa wahudumu ambao watapelekea wateja vyakula mezani.

Vilevile, wateja lazima wanawe mikono kabla kuingia.

“Kama wahudumu watakuwa hawajapimwa corona, mkahawa wako hautafunguliwa. Masharti yote lazima yafuatwe,” akasema katika kikao cha wanahabari Nairobi.

Ijapokuwa mikahawa itakuwa ikifunguliwa tu kati ya saa kumi na moja asubuhi hadi saa kumi jioni, wateja wataruhusiwa kununua pombe mkahawani.

“Pombe itauzwa pamoja na chakula ndani ya mkahawa na itakuwa kwa wateja wanaosubiri kupakuliwa chakula, wanaokula au dakika 30 baada ya mteja kumaliza kula,” akasema Bw Kagwe.