• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
WASONGA: Serikali sasa haina budi ila kuahirisha mitihani

WASONGA: Serikali sasa haina budi ila kuahirisha mitihani

Na CHARLES WASONGA

HATUA ya serikali ya kuongeza muda wa utekelezaji wa amri ya watu kutoingia na kutotoka kaunti za Nairobi, Mombasa, Kwale, Mandera na Kilifi kwa siku 21 zaidi pamoja na kafyu, imeongeza wasiwasi zaidi katika sekta ya elimu ya msingi.

Wiki iliyopita kumeibuka mjadala miongoni mwa wazazi, walimu, vyama vya kutetea masilahi ya walimu na serikali kuhusu iwapo mitihani ya kitaifa inafaa kuahirishwa au la.

Kuendelea kufungwa kwa kaunti tano nchini kwa siku siku 21 zaidi kutokana na ongezeko la maambukizi ya Covid-19, kunamaanisha kuwa kalenda ya masomo itaendelea kuvurugwa.

Ni wazi kuwa muhula wa pili ambao, kwa mujibu wa kalenda hiyo unapasa kuanza Mei 4, hautaanza kwa sababu siku ya mwisho ya marufuku hii ni Mei 16, 2020.

Huku ikionekana wazi kwamba hatua zinazotekelezwa kudhibiti corona zitavuruga maandalizi ya watahiniwa, serikali imesimama kidete kwamba mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) na ule wa kidato cha nne (KCSE) itaendelea ilivyopangwa.

Juzi, Waziri wa Elimu Profesa George Magoha alishikilia kuwa hamna haja ya kuahirishwa kwa mitahani hiyo.

Ajabu ni kwamba Rais Uhuru Kenyatta alionekana kuunga mkono kauli hiyo akisema mitihani hiyo haitasongezwa akisema serikali itatoa mwelekeo kuhusu jinsi wanafunzi wa darasa la nane na kidato cha nne watafidia muda waliopoteza.

Kwa kuwa idadi ya wanaoambukizwa Covid-19 inaendelea kuongezeka kila siku, uwezekano wa kupatikana haraka kwa chanjo ukiwa finyu, na serikali ikiendelea kutumia baadhi ya shule za upili za mabweni kama vituo vya karantini, Wizara ya Elimu inapasa kuahirisha mitihani ya kitaifa.

Kwanza, ni wazi kwamba ugonjwa huu ni hatari, na unawaua wakubwa kwa wadogo, hivyo sidhani kuna mzazi atakubali kuwarejesha watoto wake shuleni kabla ya janga hili kudhibitiwa.

Na kutokana na unyanyapaa ambao sasa umehusishwa na corona, itakuwa vigumu kuwashawishi wazazi ambao watoto wao wanasomea katika shule 460 kote nchini zinazotumiwa kama karantini kuwarejesha huko. Hofu kama hiyo bila shaka itawapata walimu, ikizingatiwa kuwa bado kuna uhaba mkubwa wa vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi.

Huku Rais Kenyatta akikiri kuwa mpango wa serikali kuendeleza uchunguzi watu wengi unazongwa na changomoto ya uhaba wa vifaa, ina maana kuwa mkondo wa kuenea kwa virusi hivyo hautavunjwa hivi karibuni. Hii ndio maana itakuwa hatari kubwa kwa serikali kufungua shule, hata kwa watahiniwa pekee.

Pia serikali ijue sio watahiniwa wote wanaofaidi kutokana na vipindi vya masomo vinavyopeperushwa kupitia redio, runingana mitandao kama ambavyo Prof Magoha anadai.

Hivyo ni lazima kuwa na mpango mahsusi wa kuhakikisha masomo yataendelea kuanzia mahala ambapo yalisimama shule zilipofungwa.

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

You can share this post!

NGILA: Vijana wakome kufanyia mzaha janga la virusi hatari

Matumaini huku waliopona corona wakifika 124

adminleo