Bingwa wa ujasiri wa kuzungumza na kujieleza mbele ya umma
Na MAGDALENE WANJA
ILI kufanikiwa katika biashara, mawasiliano bora ni mojawapo ya vitu muhimu sana.
Ni kwa sababu hii Bw Maxwell Gichuhi alianzisha kampuni ya kutoa mafunzo ya jinsi ya kuwasiliana akilenga kampuni na biashara mbalimbali.
Kulingana na Bw Kihara, hii ni mojawapo ya mbinu ambazo kampuni zinazofanya vizuri zimekuwa zikifuatilia.
Kampuni yake kwa jina Maxwell Gichuhi Consulting imekuwa ikitoa mafunzo, sio tu kwa kampuni na mashirika bali hata kwa watu binafsi ambao wanataka kupata ujasiri wa kujieleza mbele ya umma.
“Nimekuwa nikiendesha biashara ya kampuni hii pamoja na nyingine ya uchapishaji kwa muda wa miaka 15 sasa,” anasema.
Kulingana na Bw Gichuhi, mtu anapojifunza jinsi ya kuwasiliana vyema, huwa anapata faida nyingi zikiwemo kupanda cheo na hadhi katika jamii.
Anaongeza kuwa kuna baadhi ya viongozi wakuu serikalini ambao wana mawazo mema na mipango yenye faida kwa wananchi ila hawawezi kujieleza.
“Baadhi ya viongozi wana ujuzi mwingi ambao unaweza kuleta mabadiliko ila hawawezi kujieleza na kuwasilisha mawazo yao,” alisema Bw Gichuhi.
Kupitia kampuni yake, Gichuhi hutoa huduma hiyo kwa watu kati ya 15 na 20 kila mwezi; ikiwa ni idadi aliyoiweka ili kumwezesha kutoa huduma bora.
“Awamu moja ya mafunzo huchukua muda wa wiki nane ambapo hulipiwa kati ya Sh28,000 na Sh35,000,” akasema Bw Gichuhi.
Malipo hayo hata hivyo hutegemea na chaguo la kinachotakiwa na mwanafunzi mwenyewe ambapo kuna wale hutaka mafunzo ya kipekee ambayo malipo yake huanzia Sh65,000 na kuendelea.
Huduma hii hutolewa kwa ushirikiano na baadhi ya watu ambao hutoa huduma mbalimbali ili kukamilisha kukamilika kwa funzo.
Kutokana na mkurupuko wa ugonjwa wa Covid-19, Bw Gichuhi amekuwa akitoa huduma hiyo kupitia mtandaoni.