• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 9:41 AM
AGUERO: Wachezaji wanaogopa kurejelea EPL

AGUERO: Wachezaji wanaogopa kurejelea EPL

Na CHRIS ADUNGO

MFUMAJI wa Manchester City nchini Uingereza, Sergio Aguero, amesema kwa wachezaji ‘wanahofia’ kurejea uwanjani kusakata mpira wakati huu ambapo janga la virusi vya corona halijadhibitiwa vilivyo katika takriban mataifa yote duniani.

Msimu huu wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ulitarajiwa kuendelezwa mnamo Juni 8, hali ambayo ingehitaji wachezaji kurudi mazoezini kikamilifu kufikia Mei 18.

Vinara wa vikosi vyote 20 vya EPL wanatazamiwa kukutana leo Ijumaa ya Mei 1, 2020 kujadili njia mbalimbali za kurejelewa kwa kampeni za muhula huu.

“Wachezaji wengi wanaogopa kurejea uwanjani kwa sababu wana watoto na familia ambazo zinawategemea pakubwa,” akasema Aguero, 31.

Akihojiwa na runinga ya El Chiringuito nchini Argentina, Aguero aliongeza: “Ninaogopa sana. Hata hivyo, niko hapa na mchumba wangu, kwa hivyo sitatagusana na watu wengi. Nimejitenga nyumbani na mchumba wangu ambaye nadhani, ndiye mtu wa pekee ninayeweza kumuambukiza iwapo nitapata virusi hivi uwanjani,” akasema nyota huyo wa zamani wa Atletico Madrid.

“Wachezaji wengi wanasema kuna watu walio na virusi vya corona ila hawaonyeshi dalili zozote za ugonjwa huo. Itakuwa rahisi sana kwa watu kuambukizana iwapo hali itakuwa hivyo. Hiyo ndiyo sababu nimesalia hapa nyumbani. Huenda hata iwe kwamba nina virusi vyenyewe ila nisijue,” akasema mvamizi huyo wa timu ya taifa ya Argentina.

Kipute cha EPL kiliahirishwa tangu Machi 13, 2020 kutokana na virusi vya corona. Ingawa hivyo, klabu zote zimepania kusakata mechi zote 92 zilizosalia msimu huu kufikia Juni 30.

Mechi zote zinatarajiwa kusakatiwa ndani ya viwanja vitupu bila mashabiki huku baadhi zikipeperushwa moja kwa moja runingani.

Aguero anasema, “itamlazimu yeye na wenzake kuwa makini zaidi japo huenda wasiwezeshwe kumudu ukubwa wa kiwango cha wasiwasi watakapotakiwa kurejea ugani kwa minajili ya mazoezi ya pamoja kisha kuendeleza kampeni za msimu huu katika EPL, Kombe la FA na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA),”

Iwapo mazoezi ya vikosi vyote vya EPL yatarejelewa kabla ya kanuni za kutokaribiana kwa watu hazijalegezwa, huenda wachezaji wote wa kipute hicho wakafanyiwa vipimo vya afya mara mbili kwa wiki huku ukaguzi wa dalili za corona ukiendeshwa kwa kila mchezaji kila siku.

Mbali na masharti hayo, watatakiwa kuwasili katika viwanja vyao vya mazoezi wakiwa ndani ya jezi na kuvalia barakoa nyakati zote.

Aidha, hawataruhusiwa kuonga wala kula katika maeneo yoyote ya viwanja hivyo. Iwapo klabu husika zitataka kuwapa wachezaji wao vyakula, basi zitaruhusiwa kufanya hivyo kwa wanasoka kupelekewa katika magari yao na kujibebea na kwenda navyo.

Ni matibabu ya dharura pekee na yanayostahili ndiyo yatatolewa kwa mchezaji yeyote uwanjani huku maafisa wa afya watakaomshughulikia wakihitajika kuvalia mavazi rasmi ya kujikinga dhidi ya corona kuanzia kichwani hadi miguuni.

Mikutano yote ya kurejelea video za mechi na kujadili mbinu za kukabiliana na wapinzani itaandaliwa kutumia mitandao.

Kufikia sasa, ni Arsenal, Brighton na West Ham United pekee ndio wameruhusu wachezaji wao kurejelea mazoezi kikamilifu katika viwanja vyao.

You can share this post!

PSG watawazwa mabingwa wa ligi kuu ya Ufaransa

Wafanyakazi wa mikahawa kupimwa corona kwa Sh2,000

adminleo