Wafanyakazi wa mikahawa kupimwa corona kwa Sh2,000
Na CHARLES WASONGA
WAMIKILI wa mikahawa na hoteli wamepata afueni kidogo baada ya Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kutangaza kuwa watatozwa ada kati ya Sh2,000 na Sh4,000 kwa kila mmoja wa wafanyikazi wao kupimwa Covid-19.
Bw Kagwe aliiambia Kamati ya Bunge kuhusu Sheria Mbadala Alhamisi kwamba uamuzi wa kupunguza gharama hiyo ya upimaji katika hospitali za umma ulifikiwa baada ya wafanyabiashara hao kulalamika kuwa hospitali za kibinafsi zinatoza ada za juu za hadi Sh10,500 kupima mtu mmoja.
Kwa mfano, Nairobi Hospital inatoza ada ya Sh10,000 kwa kila mtu kupima Covid-19.
“Sasa tumeamua kwamba ili kutimiza mahitaji mapya kabla ya mikahawa na hoteli kuruhusiwa kuhudumu hospitali za serikali zitatoa huduma za kuwapima wahudumu kwa ada ya kati ya Sh2,000 na Sh4,000 kulingana na hadhi ya hospitali ya umma,” Waziri akaiambia Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Narok Kaskazini Moitalel Ole Kenta.
Mnamo Jumanne Serikali iliiruhusu mikahawa kufungua lakini kwa masharti makali yanayolenga kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona, kama vile wahudumu wa biashara hizo kupimwa kubaini hali yao ya afya.
Wenye mikahawa na hoteli pia walitakiwa kuhakikisha kuwa wateja na wafanyakazi wanadumisha kanuni ya kutengana kwa umbali wa mita moja, kuwekwa kwa maeneo ya watu kunawa au kutumia vieuzi (sanitizers), wateja kupimwa joto, wamikili kuchukua kibali mpya kutoka kwa idara ya afya ya umma, miongoni mwa mahitaji mengine.
Lakini wamiliki wa mikahawa na hoteli wamelalamikia gharama ya juu ya kutimiza masharti hayo kama vile wafanyakazi kupimwa virusi vya corona na ununuzi wa vifaa kama vipima joto.
“Ili kutimiza masharti haya kwa wastani, wanachama wetu wadogo watahitaji Sh500,000 huku wale wakubwa watahitaji Sh2 milioni kutimiza masharti hayo magumu,” akasema Mike Macharia ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Mikahawa na Hoteli.
“Mbona serikali haijaamuru kwamba wahudumu wa maduka ya jumla wapimwe Covid-19 ilhali maduka haya pia huuza vyakula?” Bw Macharia akauliza.
Bw Kagwe aliwaambia wabunge kwamba uamuzi wa serikali wa kuruhusu kufunguliwa kwa mikahawa ni kwa lengo la kupunguza athari za Covid-19 kwa uchumi wa nchi.