RIZIKI: Hali mbaya tuktuk
Na SAMMY WAWERU
JOSEPH Kago ni dereva na mhudumu wa tuktuk eneo la Githurai kiungani mwa jiji la Nairobi, mojawapo ya sekta inayolia kuathirika kwa kiwango kikuu na janga la corona.
Ameajiriwa, na jioni anapokunja jamvi shughuli za siku, sharti ampe mmiliki kilicho chake.
Ni mume na baba wa mtoto mmoja na analia mapato ya siku jumla hayatoshi kulipa mwajiri wake na kukidhi mahitaji ya familia yake.
“Huduma za tuktuk zimeathirika pakubwa na Covid-19. Ugonjwa huu umesababisha kushuka kwa mapato yetu kwa kiwango kikubwa. Mimi ndiye tegemeo katika familia yangu,” Kago aelelezea, akitafakari jinsi gani atakavyoweza kukimu familia yake hali ikiendelea hivi.
Amekuwa katika sekta hiyo ya uchukuzi kwa takriban miaka mitano, na anasema ikiwa amewahi kupitia magumu maishani, athari za virusi vya corona zimevuka mipaka.
Tunampata akiwa kwenye foleni ya vijigari hivyo vidogo katika steji ya Githurai, vinakohudumu kati ya mtaa huo na Progressive, Mumbi, Mwihoko na barabara ya hivi karibuni kuzinduliwa ikiwa Mwiki.
Awali, nauli mitaa karibu na Githurai haikuzidi Sh20, lakini kufuatia chimbuko la Covid – 19 nchini wahudumu hao walilazimika kuongeza Sh10 zaidi, ikiwa na maana kuwa haipungui Sh30. Kati ya mtaa wa Githurai na Mwihoko, abiria wanalipa Sh50, kutoka Sh30 na 40, ada hizo zikitegemea nyakati za siku.
Kwenye laini akisubiri kupakiwa abiria inamchukua zaidi ya dakika thelathini, shughuli ambayo awali haikuzidi dakika 10 au robo saa.
“Si ajabu kukawia hapa saa nzima tukisubiri wateja wafike. Wamepungua kwa kiasi kikuu, wengine wakitembea kwa miguu ili kuokoa pesa na hofu ya kuambukizwa corona,” Kago anaiambia ‘Taifa Leo’.
Kutia msumari moto kwenye kidonda kinachouguza, muda huo wote anasubiri kupakiwa abiria wawili pekee. Hii ni kutokana na amri ya serikali matatu zote na tuktuk zisisafirishe zaidi ya asilimie 60 ya watu mara moja.
Mwezi Machi 2020 Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alitoa taratibu na sheria katika sekta ya uchukuzi, ambapo jumla idadi ya abiria wanaobebwa mara moja ilishushwa, wahudumu wa bodaboda nao wakitakiwa kusafirisha abiria mmoja na wote wawe na barakoa, ili kuzuia usambaaji wa Covid-19.
Waziri Kagwe pia aliamuru kila abiria kwenye matatu, tuktuk na bodaboda, sharti avalie maski.
Wahudumu wa tuktuk Githurai wametii amri ya serikali, kila kijigari kikiwa na vitakasa mikono, ambapo abiria ananawishwa mikono kabla ya kuingia. Mwelekeo wote wa serikali ili kuzuia maambukizi ya corona, wameutilia maanani, ila wanalalamikia kukosa mapato.
Madereva walioajiriwa, kabla ya kisa cha kwanza cha corona kutangazwa nchini, tuktuk nyingi walikuwa wakilipa wamiliki Sh1,000 kwa siku, gharama ya mafuta ikiegemea upande wa dereva.
Kafyu ya usiku ilipotangazwa mwezi uliopita, Joseph Kago anasema biashara hiyo ilididimia mara moja, mshahara waliopaswa kulipa ukiwa vigumu kuafikia.
Hata ingawa muungano unaosimamia sekta hiyo – Githurai Tuktuk Association GTA – ulirai wamiliki kuwapunguzia kati ya asilimia 30 na 40, John Kinuthia anasema kupata mshahara huo umekuwa sawa na kupanda mlima kwa kandambili.
“Tuktuk inapaswa kusafirisha abiria watano, idadi hiyo ilishushwa hadi wawili ili kuzingatia umbali kati ya mtu na mwenzake. Hebu jiulize, kusafirisha abiria wawili kila awamu mmoja akilipa Sh30, na kuzidisha maji kwenye unga hawapatikani, nitajaza lini Sh600 au Sh700 za mmiliki?” ahoji dereva huyo.
Ikizingatiwa kuwa gharama ya mafuta ni yake, Kinuthia anasema kusalia na Sh300 kwa siku ni kwa neema ya Mungu.
“Mapato hayo ndiyo riziki ya familia na kodi ya nyumba,” aeleza, akishangaa atakavyoweza kukimu familia mambo yasipoimarika.
Kauli ya mhudumu huyo inapigwa jeki na Edwin Mwangi, ambaye pia ni dereva, akisema kwake chakula kinacholiwa ni kiamsha kinywa na cha jioni pekee. “Inabidi tunajinyima ili watoto wale,” Mwangi anasema.
Isitoshe, kuna baadhi ya tuktuk zilizonunuliwa kwa mikopo hivyo basi wamiliki wanasubiri mshahara siku ikikamilika endapo gari lake litashinda barabarani.
Mtaa wa Githurai una zaidi ya tuktuk 300 na madereva wanaomba wamiliki kuwashushia bei zaidi.
Janga la corona limekitisa ulimwengu mzima, sekta ya biashara, watu kupoteza kazi, wengine kusimamishwa kwa muda na kupunguzwa mishahara vikiwa visa vinavyoripotiwa.
Kimsingi, Covid-19 imeathiri uchumi kwa kiwango kikubwa, wataalamu wakionya wananchi watarajie nyakati ngumu ikiwa janga hili halitadhibitiwa.
“Hali inavyoonekana, huenda wananchi hasa wafanyabiashara watakuwa na wakati mgumu kufufua biashara zao,” Dennis Muchiri, mtaalamu wa masuala ya biashara na uchumi anaelezea.
Sekta za biashara ndogondogo na za kadri, pamoja na juakali zimeathiriwa pakubwa.
Muchiri anapendekeza serikali iibuke na mikakati kuzipiga jeki mara janga la corona litakapokuwa limedhibitiwa kikamilifu.