Makala

Jinsi wazee wa Agikuyu walivyofanya tambiko dhidi ya Covid-19

May 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

WAZEE wa Agikuyu wapatao 15 walifanya tambiko katika Mto Chania, Thika, kwa lengo la kufukuza maradhi ya Covid-19.

Wakiongozwa na mzee Bw James Njoroge, wazee hao walisema walimchinja mbuzi na kumchoma hadi kuwa majivu.

“Hatua hiyo ni ya kuhakikisha tunafukuza pepo mbaya, maradhi ya Covid-19 ambayo yamesababisha shughuli nyingi kusitishwa ulimwenguni kote,” alisema Bw Njoroge.

Wazee hao walitoa mwito kwa viongozi wote waungane ili kupambana na janga hilo la corona kwa pamoja.

Hafla hiyo iliendeshwa kando ya Mto Chania mjini Thika, mnamo Alhamisi.

Alisema tambiko hilo lina sheria yake muhimu kwamba kabla ya kutekeleza wajibu huo ni sharti wazee wanaohusika kufunga na kusali kwa siku saba mfululizo.

Baada ya kufunga, wazee watatu wananunua mbuzi maalum ambaye hutolewa kama kafara.

Walisema janga la corona limesababisha wasiwasi mwingi nchini na ulimwenguni kote.

Walisema mara baada ya mbuzi huyo kuchomwa, wanakusanya majivu hayo yote na masalio yote ya moto na kuyatupa katika mto huo wa Chania ili kufukuza ‘pepo’ na corona.

“Kabla ya kuanzisha hafla hiyo kwanza wazee hao wamefanya maombi maalum ili kujiandaa rasmi kumchinja mbuzi huyo ambaye alikuwa amefungwa kwa kamba kando ya moto unaowaka,” alisema Bw Njoroge.

Alisema jambo walilolifanya sio geni kwa sasa kwa sababu hata miaka ya hapo nyuma kulikuwa na magonjwa ya aina nyingi kama gatema, munyero, upele, na hata polio na yote wazee waliyafanyia matambiko wakati huo,” alisema Bw Njoroge.

Bw Ng’ang’a Kamuyu, ambaye ni mmoja wa wazee walioendesha tambiko hilo anasema anatoka katika mbari ya Merie, na ameona mengi yakifanywa na wazee.

“Tunataka tupambane na corona vilivyo hadi tuone tumeisukuma katika maji mkuu ya Bahari Hindi. Lengo letu ni kufanya tambiko na kumuomba Mungu aiangamize kabisa corona,” alisema Bw Kamuyu.

Matumaini

Aliwapa matumaini Wakenya kwa kusema ya kwamba janga hilo litapotea na watu kurejelea kazi zao za kawaida.

“Kila mmoja anastahili kumtegemea Mungu na kuomba kwa bidii ili tuangamize jinamizi hilo. Ni sharti tupige magoti na kumuomba,” alisema Bw Kamuyu.

Wazee hao walitengeneza mduara na kuweka moto wao katikati kwa lengo la kutekeleza tambiko hiyo.

Walitoa mwito kwa wakenya wote popote walipo wafuate sheria zote zilizowekwa na serikali zikiwemo kunawa mikono kila mara, kuvalia barakoa, na cha muhimu zaidi kujitenga kwa umbali wa mita chache baina ya mtu na mwenzake.

“Iwapo tutafuata masharti hayo yote bila shaka janga hilo litadhibitiwa kwa kiwango kikubwa. Watu wengi kwa sasa wanapitia hali ngumu ya maisha,” alisema mzee huyo wa Agikuyu.