Polisi kutenga vituo vipya vya karantini kwa wanaokiuka kafyu
Na CHARLES WASONGA
WALE wanaovunja sheria ya kafyu sasa watakuwa wakizuiliwa katika vituo vya karantini vilivyotengwa na serikali na tena katika vituo maalum.
Waziri Msaidizi wa Afya Rashid Aman alitangaza Jumapili kuwa Kamati ya Kitaifa ya Dharura Kuhusu Covid-19 imemwagiza Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai kutenga maeneo maalum ambako wavunjaji sheria na kanuni watazuiliwa.
“Na katika maeneo hayo sheria inayohimiza watu kutokaribiana itazingatiwa kwa makini ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona,” Dkt Aman akasema alipokuwa akitoa taarifa ya kila siku kuhusu hali ya janga la corona nchini, jijini Nairobi.
Waziri huyo msaidizi alitangaza kuwa kwa mara ya kwanza tangu kisa cha kwanza cha ugonjwa huo kuripotiwa nchini mnamo Machi 13, 2020, Kenya imeandikisha visa 30 ndani ya muda wa saa 24 baada ya sampuli zaidi ya 800 kupimwa.
Kufikia Jumapili Kenya ilikuwa imethibitisha jumla ya visa 465 tangu Machi 13.
Kumekuwa na malalamishi kutoka kwa umma kwamba polisi wamekuwa wakiwakamata wanaokiuka sheria za kafya na kupelekwa katika vituo vya karantini ambapo wanawekwa pamoja na watu ambao huenda wana ugonjwa wa Covid-19.
Hali hiyo, wanasema, inawaweka watu wengine katika hatari ya kuambukizwa na hivyo kuhujumu vita dhidi ya janga hilo.
Zaidi ya hayo watu hao hulazimishwa kugharimia huduma duni katika vituo hivyo licha ya kwamba ni taasisi za serikali kama shule.
Hii ndiyo maana katika mwezi Aprili kulitokea visa viwili vya watu kutoroka kutoka kwa vituo vya karantini katika kaunti ya Nairobi na ile ya Mandera.
Kisa cha kwanza kilitokea katika Chuo cha Ufundi cha Mandera ambapo watu 32 miongoni mwa wale waliozuiliwa hapo walitoroka.
Kisha mnamo Aprili 22, 2020, watu 50 waliokuwa wamezuiliwa katika Chuo cha Mafunzo ya Utabibu (KMTC) Nairobi walitoweka kuwa kuruka ua la taasisi hiyo.