Polisi wachunguza chanzo cha kifo cha Tecra Muigai
Na KALUME KAZUNGU
POLISI Kaunti ya Lamu wanaendeleza uchunguzi kuhusiana na kifo cha Bi Tecra Muigai ambaye ni binti wa mmiliki wa Kampuni ya Pombe na Mvinyo ya Keroche Breweries, Bi Tabitha Karanja aliyefariki Jumamosi.
Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo unaashiria kuwa Bi Tecra alifariki kutokana na majeraha mabaya ya kichwa aliyopata baada ya kuanguka kutoka kwa ngazi za nyumba aliyokuwa amekodi na kuishi na mpenziwe kwenye mtaa wa kifahari wa Shella, kisiwani Lamu takriban juma moja lililopita.
Kufikia Jumapili, rafiki ya marehemu aliyetambuliwa kwa jina Omar Lali tayari alikuwa amekamatwa na maafisa wa usalama ili kuendeleza uchunguzi kuhusiana na utata unaozingira kifo cha mwanadada huyo wa kutoka familia maarufu.
Marafiki wa karibu wa Bi Tecra waliozungumza na Taifa Leo na kudinda kutaja majina yao wamesema mwendazake amekuwa akiishi Lamu kwa takriban wiki tatu hasa tangu alipomtembelea mwanamume huyo mapema Aprili.
Ukuruba wa Bi Tecra na Lali – ambaye kazi yake ni kutoa huduma za watalii wanaozuru ufuo wa bahari eneo la Lamu – ulianza katikati ya mwaka 2019 na wamekuwa wakionekana kwenye maeneo ya burudani wakijivinjari kwa vinywaji.
Pia inadaiwa Lali hupenda sana kutafuna miraa.
“Tunasikitika kwamba Bi Tecra alifariki kutokana na majeraha aliyopata hapa Lamu ambapo alianguka kutoka kwa ngazi za ghorofa ya nyumba alimokuwa akiishi na mpenzi wake eneo la Shella,” akasema mmoja wa marafiki zake walioko Lamu.
Amebainisha kwamba mara baada ya kuanguka alivuja damu kwenye mdomo na mianzi ya pua na pia alipoteza fahamu.
Kwamba ilibidi simu zipigwe haraka kwa mamake jijini Nairobi, ambapo alituma ndege ya binafsi iliyomchukua kwenye uwanja mdogo wa ndege hapa Lamu na kumkimbiza hospitalini Nairobi kwa matibabu.
“Tumehuzunishwa na kifo chake.”
Mmoja wa maafisa wa polisi anayehusika na uchunguzi wa tukio hilo amedokeza kwamba Lali ndiye mshukiwa wa kwanza katika tukio la ajali lililosababisha majeraha na kifo cha Bi Tecra.
“Tumemkamata Omar Lali ambaye ni rafiki yake Bi Tecra na kwa sasa huyo ndiye mshukiwa wetu mkuu katika uchunguzi tulioanzisha. Hivi tunavyozungumza tuko kwenye nyumba ambako binti anadaiwa alianguka kutoka ngazini. Tunataka kujua hasa ni vipi marehemu alianguka na chanzo chake. Tunakisia kuna jambo linafichwa hapa,” akasema afisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Kwa upande wake aidha, Kamanda wa Polisi, Kaunti ya Lamu, Bw Moses Murithi amesema ni kweli uchunguzi umeanzishwa kuhusiana na madai kwamba Bi Tecra alianguka kwenye nyumba moja mtaa wa Shella, kisiwani Lamu.
“Tuwape polisi nafasi kutekeleza uchunguzi. Kwa sasa siwezi kusema dhahiri kwamba ni kweli mwanadada huyo alianguka na kupata majeraha Lamu kwa sababu ripoti ya kwanza kuhusiana na tukio hilo ilifanywa Nairobi. Uchunguzi unaendelea,” akasema Bw Murithi.