Chama cha maslahi ya wanasoka chataka majadiliano kabla mishahara kupunguzwa
Na CHRIS ADUNGO
CHAMA cha Maslahi ya Wanasoka Nchini (KEFWA) kimewataka vinara wa klabu za Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kushauriana vilivyo na wachezaji wao kabla ya kufikia maamuzi ya kupunguza mishahara yao.
Katika taarifa yake, KEFWA imesisitiza kwamba zipo baadhi ya klabu ambazo zimepuuza maslahi ya masogora wao katika kipindi hiki ambapo ulingo wa michezo umetikiswa pakubwa na janga la corona.
Licha ya mazungumzo ya awali kati ya vinara wa KEFWA na wasimamizi wa vikosi vyote vya KPL, wengi wa wachezaji hawajahakikishiwa na waajiri wao kuhusu malipo na kiasi cha mshahara watakaokuwa wakilipwa hadi janga la corona litakapodhibitiwa vilivyo.
“Tulizungumza na vinara wa KPL kwa lengo la kuanzisha mikakati na mpangilio wa kuwafaidi kifedha wachezaji ambao wameathiriwa na virusi vya corona huku vikosi husika vikisalia na fedha za kutosha kujiendesha,” ikatanguliza taarifa ya KEFWA.
“Ni matumaini yetu kwamba vikosi vyote vitashauriana kwa kina na wachezaji wao na kufikia mwafaka utakaoepusha matukio ambapo wanasoka wanavutana na waajiri wao kuhusu malipo,” akasisitiza mwenyekiti wa KEFWA, James Situma.
Hadi kufikia sasa, ni klabu za KCB na Wazito FC pekee ambazo zimetoa hakikisho kwa wachezaji wao kwamba wataendelea kupokea mishahara yao yote jinsi ilivyokuwa hapo awali kabla ya kushuhudiwa kwa mlipuko wa virusi vya homa kali ya corona.
Taarifa ya KEFWA inatolewa siku chache baada ya kikosi cha Western Stima kupunguza mishahara ya wachezaji wake katika mwezi wa Aprili 2020 kwa hadi asilimia 50.
Wanasoka wengi wa Stima ambao walitaka majina yao yabanwe, wamesema kwamba hatua iliyochukuliwa na usimamizi wa klabu yao iliwajia kwa mshangao mkubwa.
Hata hivyo, vinara wa kikosi hicho kinachodhaminiwa na kampuni ya umeme ya Kenya Power & Lighting, wameshikilia kwamba bajeti iliyotolewa kwa minajili ya matumizi ya msimu huu wa 2019-20 inaelekea kukatika na klabu inakabiliwa na uchechefu mkubwa wa fedha.
Katika mjadala ulioandaliwa kati ya usimamizi na wanasoka wa Stima mnamo Februari 2020, wachezaji walipendekeza kukatwa asilimia 10 ya mishahara yao japo klabu ilishikilia msimamo wa kunyofoa ujira huo kwa hadi asilimia 30.
“Hakuna yeyote ambaye amefurahia maamuzi haya ambayo mwanzo, yamechukuliwa bila ya mwafaka wowote kupatikana. Kupunguziwa nusu ya mshahara katika kipindi hiki kigumu si jambo rahisi,” akasema mmoja wa wachezaji kwa kusisitiza kwamba wengi wao wamejiondoa katika kundi la WhatsApp la kikosi cha Stima kutokana na hatua hiyo ya usimamizi.
Kwa upande wake, Laban Jobita ambaye ni mwenyekiti wa Stima alisema, “Hili ni suala la ndani kwa ndani ambalo sitaki kujadili kwa sasa kwenye vyombo vya habari.”
Hadi Ligi Kuu ya KPL iliposimamishwa mwanzoni mwa Machi 2020 na Gor Mahia kutawazwa mabingwa wiki hii, Stima walikuwa wakishikilia nafasi ya saba kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 36.
Stima inakuwa klabu ya pili ya KPL baada ya Kakamega Homeboyz kupunguza mshahara wa wachezaji wake baada ya kulipuka kwa corona.
Mnamo Machi 29, 2020, Afisa Mkuu Mtendaji wa Homeboyz, Bernard Shitiabayi, alisema kwamba wachezaji wao walikubali kupungiziwa posho kwa hadi asilimia 50.
Hii ilikuwa baada ya wadhamini wao, Serikali ya Kaunti ya Kakamega, kunyofoa ujira wa wafanyakazi wake kwa kati ya asilimia 10 na 30 kwa kipindi cha miezi mitatu.