Akanusha shtaka la kutumia mabavu kunyang'anya mkazi wa Nairobi mkufu wa dhahabu
Na RICHARD MUNGUTI
TAMAA ya kujipatia fedha kwa njia ya haraka ilisababisha mwanaume mwenye umri wa miaka 35 kukanyaga kizimba cha mahakama ya Milimani, Nairobi.
Brandon Njuguna Ng’ethe ambaye ni pandikizi la mtu alishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Bi Zainab Abdul.
Brandon alikana shtaka la kumnyang’anya kimabavu Samuel Otieno Omuga mkufu wa dhahabu ulio na thamani ya Sh55,000.
Shtaka lilisema Brandon alitekeleza uhalifu huo katika barabara ya Moi Avenue, Nairobi mnamo Mei 4, 2020.
Alikanusha shtaka dhidi yake na kuomba aachiliwe kwa dhamana akieleza hakimu mwandamizi Zainab Abdul kwamba ni haki yake kuachiliwa huru.
Kiongozi wa mashtaka hakupinga ombi hilo.
Bi Abdul alimwachilia kwa dhamana ya Sh70,000 pesa taslimu na kuamuru kesi hiyo itajwe Mei 20 kwa maagizo zaidi.
Mshtakiwa huyo mwenye misuli laini kama mnyanyuaji uzani anakabiliwa na shtaka ambalo akipatikana na hatia ama atahukumiwa kunyongwa au akabidhiwe kifungo cha maisha gerezani.
Hakimu aliamuru mshtakiwa asukumwe jela endapo hatalipa dhamana hiyo.
Hakimu aliamuru mshukiwa asalie rumande aliposhindwa kuilipa dhamana hiyo.
Kesu ilitengwa itajwe mnamo Mei 20 itengewe siku ya kusikizwa.