• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Alama ya kistari kifupi, ritifaa na nuktakatishi katika uakifishaji

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Alama ya kistari kifupi, ritifaa na nuktakatishi katika uakifishaji

Na MARY WANGARI

HUTUMIKA kama alama ya hisabati na kisayansi kuonyesha tarakimu au kiwango cha chini ya sufuri 0.

Kwa mfano:

Kiwango cha baridi kimeshuka hadi -5 digrii C.

-2-2= -4

Kuonyesha tarehe

Watu wengi walikufa katika vita vya baada ya uchaguzi 1997-1998

Mshindi alirejea nchini tarehe 05-12-2019

Alama ya Apostrofi, ritifaa, (‘) katika uakifishaji

Kituo hiki cha uakifishaji hutumika kwa njia zifuatazo:

Alama ya ritifaa hutumika kuonyesha utamkaji wa nazali au ving’ong’o. Kwa mfano:

Ng’ang’ania

Ng’arisha

Ng’ata

Nong’ona

Ng’ombe

Ng’atuka

Ng’ambo

Kituo cha apostrofi pia hutumika kuashiria herufi, nafasi au tarakimu iliyoachwa kwa mfano:

’19= 2019

N’shakwambia – nimeshakwambia

N’siende – nisiende

Huonyesha utamkaji wa nazali au ving’ong’o

Alama ya dukuduku, nuktakatishi (…) katika uakifishaji

Kituo hiki kwa kawaida hutumia nukta tatu au zaidi zinazofuatana.

Kituo hiki huonyesha dukuduku la usemi uliokatishwa na hutumika kwa usemi uliokatishwa lakini unaojulikana kwa wengi; mathalan kibwagizo, nahau, methali na kadhalika.

Fuata nyuki … (Methali)

Ganda la mua la jana …

Kituo cha nuktakatishi vilevile hutumiwa kuonyesha mazungumzo, maelezo na maneno mengine.

Kituo cha nuktakatishi hutumika kuonyesha maneno yaliyochanganyika na hali ya kuvuta maneno, kuvuta subira, kuibua taharuki au hali ya kusitasita katika tabia ya msemaji.

Kwa mfano:

· Kuonyesha maelezo, mazungumzo, n.k. yaliyochanganyika na hali ya kuvuta maneno au kuvuta subira katika tabia ya msemaji.

Kwa mfano:

Ghafla bin vuu, tulisikia usiyahi mkali…(taharuki)

Ni…nili…mwona akitorokea kichakani (kigugumizi)

Sote tulipiga goti moja chini huku firimbi ikipulizwa:moja…mbili…tatu…! (mashindano ya riadha)

Aidha, kituo cha ritifaa hutumika kuashiria kwamba kuna maneno yaliyotagulia au yanayoendelea kando nay ale yaliyokaririwa.

Kwa mfano:

…wakora na wadhalimu ndio wanaoonekana kuendewa vyema ; watu wakarimu na waaminifu utawaona waking’ang’ana

…Wabunge wataanza vikao vyao mara tu baada ya likizo kukamilika.

Alama ya dukuduku pia hutumika kuonyesha kuwa katika sentensi iliyoandikwa kuna baadhi ya maneno ambayo yamekatishwa.

Wajua ya dunia, leo mimi …

Huonyesha maelezo yanayotolewa yanavutwa. Kwa mfano:

kwenye mstari…

kaa tayari …

nenda …

Hutumiwa kuonyesha sentensi isiyokamilika

Kama haya ndiyo maisha, mimi …

[email protected]

Marejeo

Mkinga, M.G. (2007). Kiswahili kwa Shule za Msingi 2 (MWL), Dar es Salaam: Educational Books Publishers Ltd.

Norton, S. & Green, B. (2002). Essay Essentials with Reading, Tol. 3, Edinburgh: Thomson Nelson.

Stephano, R. (2015). “Uzingatizi wa Viakifishi katika Uandishi wa Kitaaluma: Mifano kutoka Shule za Msingi Tanzania.” Tasnifu ya Shahada ya Uzamivu ya Chuo Kikuu cha Dodoma (haijachapishwa)

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Alama ya kistari kifupi, ritifaa...

SANAA: Anaimairisha viatu kwa ubora na mwonekano aupendao...

adminleo