Habari

COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 28 idadi jumla ikifika 649

May 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY WAWERU

KIPINDI cha saa 24 zilizopita Kenya imethibitisha visa 28 vya wagonjwa wa Covid-19 idadi jumla nchini ikifika watu 649 kwa mujibu wa Wizara ya Afya.

Waziri Msaidizi wa Afya Dkt Rashid Aman amesema 28 hao wamebainika baada ya wataalamu wa afya kuchukua sampuli kutoka kwa watu 1,611 na kisha kufanyiwa vipimo.

“Katika 28 hao, 24 ni Wakenya huku wanne wakiwa ni raia wa taifa jirani Tanzania,” amesema Dkt Aman.

Raia hao wanne wa Tanzania waliingia nchini kupitia eneo la mpakani Migori, ameeleza Dkt Aman akihutubu katika makao makuu ya wizara jijini Nairobi leo Jumamosi.

Amehimiza umuhimu wa madereva wa malori ya masafa marefu yanayotoka nje ya nchi kupimwa.

“Kabla kuvuka boda, waonyeshe vyeti kwamba hawajaathirika na maradhi ya Covid-19,” waziri huyo msaidizi amesema.

Katika takwimu za leo Jumamosi, visa 10 vimetoka Kaunti ya Mombasa, jiji kuu la Nairobi likisajili visa tisa na Migori visa vinne.

Kajiado imekuwa na visa viwili nazo Machakos, Kiambu na Homa Bay zikiwa na kisa kimoja kila kaunti.

“Watu watilie maanani uvaliaji maski, kunawa mikono, kuzingatia umbali baina ya mtu na mwenzake na kuepuka kukongamana,” Dkt Aman akakumbusha.

Wagonjwa watano wameripotiwa kupona, idadi jumla ya waliopona nchini ikifikia 207.

Hata hivyo, mgonjwa mmoja kutoka Mombasa ametangazwa kufariki, kisa hicho kikifisha jumla ya 30 waliofariki kutokana na Covid-19.

Ili kuzuia maambukizi zaidi, Dkt Aman amehimiza umma kujitokeza kupimwa ili mtu ajue kama ama ameathirika au la na hivyo hatua zaidi kuchukuliwa kwa lengo la kuimarisha afya.

Takwimu kutoka katika wizara zinazoangazia janga hili sasa zinaonyesha kwamba kufikia sasa sampuli 31,041 zimefanyiwa vipimo ambapo 649 matokeo yamekuwa chanya.

Aidha, waliopona ni 207 huku wahanga walioangamia kwa sababu ya maradhi haya ikipanda na kufika watu 30 nchini.