• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 5:54 PM
MWANAMKE MWELEDI: Yuko katika mstari wa mbele vita dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuiwa

MWANAMKE MWELEDI: Yuko katika mstari wa mbele vita dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuiwa

Na KEYB

TOKEA siku za ujana wake akiwa mwalimu wa shule ya upili, hadi kipindi alichohudumu katika shirika la Umoja wa Mataifa, Profesa Miriam Were amekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuiwa.

Aidha, amekuwa mtetezi wa kusaidia vijana kujitegema kupitia kwa Uzima Foundation, wakfu alioanzisha kwa ushirikiano na mumewe huku msukumo wake ukichochewa na imani yake thabiti.

Ni msimamo huu ambao ulishawishi pakubwa chaguo lake kitaaluma hasa ikizingatiwa kwamba kanisa lake lilisisitiza umuhimu wa usafi na amani, miongoni mwa masuala mengine muhimu katika jamii.

Ndoto yake ya kuwa daktari ilikatizwa kwa sababu shule yake ya upili haikuwa na maabara ya kemia na fizikia, masomo ambayo alihitaji ili kufuzu kusomea udaktari.

Hata hivyo, mara kwa mara angejitolea katika harakati za usafi katika kambi za makanisa.

Ni hapa ndipo wamishenari walitambua kipaji katika huduma ya afya ya kijamii, na hivyo kumwezesha kupata ufadhili wa masomo ya sayansi.

Alikuwa Mwafrika wa kwanza kunufaika na mpango wa mafunzo ya huduma ya afya katika Chuo Kikuu cha William Penn College nchini Amerika.

Baada ya kuhitimu alianza kusomea shahada ya udaktari lakini kutokana na kiu ya kutaka kurejea nyumbani, aliachana na kozi hiyo na kurejea nyumbani mwaka wa 1965.

Japo alitamani kusomea udaktari katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda, wakati huo serikali ya Kenya ilihitaji walimu zaidi wa sayansi, na hivyo akaamua kusomea ualimu.

Akiwa mwalimu katika mojawapo ya shule alizokuwa akifunza ndipo alipogundua kwamba wanafunzi wengi walikuwa wakipata magonjwa, na jitihada zao za kupata tiba katika hospitali za kijamii hazikufua dafu.

Ni hapa ndipo alipoamua kuacha ualimu na kusomea udaktari katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Kama daktari aidha aligundua kwamba kutokana na uhaba wa madaktari, wengi wao walilemewa na kazi nyingi suala lililosababisha vifo vingi vya watoto. Ni hapo ndipo alipoamua kushughulikia suala la afya ya umma.

Alirejelea masomo zaidi nchini Amerika na kuimarisha taaluma yake ya udaktari.

Baada ya kuhitimu, alirejea nchini Kenya ambapo aliasisi mpango wa kwanza wa kutoa shahada ya uzamili katika masuala ya afya ya umma katika Chuo Kikuu cha Nairobi huku kikosi cha kwanza cha wanafunzi kikihitimu mwaka wa 1985. Alipandishwa madaraka na kuwa mkuu wa idara ya afya ya kijamii katika chuo kikuu hicho.

Prof Were amehudumu katika mashirika na nyadhifa mbali mbali ikiwa ni pamoja na Baraza la Kitaifa kuhusu maradhi ya Ukimwi na Hazina ya utafiti wa kimatibabu barani Afrika (AMREF).

Jitihada zake zimetambuliwa kitaifa na kimataifa ambapo amepokea tuzo mbali mbali. Baadhi ya tuzo ambazo amepewa ni pamoja na Elder of the Order of the Burning Spear (EBS) mwaka wa 2005.

Aidha alikuwa wa kwanza kupokea tuzo ya Hideyo Noguchi Africa Prize mwaka wa 2006, na mwaka mmoja baadaye alipewa tuzo ya Queen Elizabeth II Gold Medal, kutokana na mchango wake kwa afya ya umma kimataifa na kuhimili mahitaji ya kiafya kwa watu maskini.

You can share this post!

Visa vya wananchi kuwapiga polisi vyaibua wasiwasi tele

SIKU YA MAMA: Selina Awinja aeleza jinsi anavyowalea wanawe...

adminleo