'Inua Mama' sasa wawatetea maseneta wa Jubilee walioitwa 'washikishwe adabu'
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE wanachama wa vuguvugu la ‘Inua Mama Jenga Jamii’ wamewataka maseneta walioagizwa wafike mbele ya kamati ya nidhamu ya Jubilee wakaidi amri hiyo.
Wakiongozwa na Mbunge wa Kandara Alice Wahome wandani hao wa Naibu Rais William Samoei Ruto badala yake wamewataka wenzao waelekea mahakamani wakiitaja kamati kama “korti ya kangaroo.”
Wameusuta uongozi wa Jubilee kwa kuwadhulumu wenzao “bila sababu maalum” ilhali walichangia pakubwa ushindi wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.
Wahome na wenzake wamekuwa wakiwahutubia wanahabari leo Alhamisi katika majengo ya bunge.
Jumatano, maseneta hao watano walifurushwa kwa kususia mkutano ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi Jumatatu.
Walioandikiwa barua za kufurushwa ni pamoja na Millicent Omanga, Falhada Dekow Iman, Naomi Jillo Waqo, Victor Prengei na Mary Seneta.
Kulingana na taarifa fupi iliyotolewa na Katibu Mkuu Raphael Tuju mnamo Jumatano, watano hao walifukuzwa kwa mienendo mibaya na kukosa heshima kwa uongozi wa chama.
“Walipokea mwaliko wa mkutano lakini hawakujali hata kuomba radhi kwa kutohudhuria,” akasema Tuju.
Hata hivyo, wandani wa Dkt Ruto katika Seneti wameshikilia hawakualikwa katika mkutano huo.
Ni katika kikao hicho kilichohudhuriwa na maseneta 20 kati ya 35 ambapo maseneta Kipchumba Murkomen na Susan Kihika, walivuliwa nyadhifa za kiongozi wa wengi na kiranja wa wengi – mnadhimu – mtawalia.