Je, ni upi mtazamo wako kuhusu uchoraji chale 'tattoo'?
Na MARGARET MAINA
HENRY Ndege, mwenye umri wa miaka 31, anashikilia ‘bunduki’ ya chale au tattoo kwa uangalifu wakati anamchora mteja wake.
Msanii huyu anajulikana sana mjini Nakuru.
Mwanzilishi na mmiliki wa studio ya Captain Lithium inayotoa huduma za uchoraji chale anasema alianza kuipenda sanaa akiwa na umri mdogo sana na kikawa kichocheo tosha cha yeye kusomea kozi ya Sanaa na Ubunifu katika chuo cha Mwangaza.
“Baba yangu marehemu alikuwa msanifuujenzi na mama yangu alikuwa mpishi na msanii. Ndugu yangu ni mchoraji na mwalimu wa sanaa,” anasema.
Baada ya kukamilisha elimu ya taasisi ya juu mnamo 2007 Henry alihamia Mombasa na kuanza kuuza picha zake karibu na Fort Jesus.
“Nilialikwa kwenye maonyesho ya sanaa yaliyoandaliwa na wizara inayohusika na utamaduni na nilikutana na Mwitaliano ambaye alikuwa na chale nyingi. Nilivutiwa na nilimwendea, nikitaka kujifunza kuhusu tattoo, ”
Henry anasema kwamba baada ya mazoezi mengi, aliichora tattoo yake ya kwanza kwa mteja na alilipisha Sh2,000.
“Ninajitahidi kujifunza kila kitu kuhusu tattoo kwani inahitaji umakinifu na kuchora picha za kudumu na muundo kwenye ngozi ya mtu sio rahisi jinsi wadhanivyo baadhi ya watu,” anasema.
Hapa anaeleza jinsi alivyofungua chumba cha huduma za chale mjini Nakuru.
“Nilihamia Nakuru mwaka wa 2015 nikiwa na akiba ya Sh300,000 kutoka uuzaji wa picha zangu, hela ambazo nilitumia kuanzisha chumba changu cha kwanza cha huduma za tattoo. Ilikuwa biashara ya kushirikiana,” anasema.
Ingawa amekuwa maarufu katika kazi yake, anasema amekumbwa na changamoto si haba; kuanzia kwa watu wenye kuihusisha sanaa hii na ‘harakati za kishetani’.
“Nina wateja kote Afrika Mashariki. Tattoo ghali zaidi ambayo nimewahi kufanya nililipisha Sh78,000; ilinichukua muda wa saa 10 kukamilisha,” anaeleza.
Kwa sasa Henry anafurahia kuwa ana pesa za kutosha kulipa bili na kusaidia familia yake.
Henry amewafundisha wanawake wengi sanaa ya uchoraji wa chale.
Anawashauri vijana waepuke lalama za kila mara kwamba kuna uhaba wa nafasi za ajira na badala yake wautumie muda wao kukuza na kuimarisha talanta zao.