Habari

COVID-19: Visa jumla Kenya vyapanda hadi 830 wahanga wakifika 50

May 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CHARLES WASONGA na SAMMY WAWERU

IDADI ya visa vya maambukizi ya virusi vya corona nchini Kenya sasa imepanda hadi 830 baada ya watu wengine 49 kupatikana na virusi hivyo.

Akihutubia taifa katika Ikulu ya Nairobi, Rais Uhuru Kenyatta, pia amethibitisha kuwa watu watano zaidi wamefariki kutokanana na Covid-19 na kufikisha 50 idadi ya waliongamizwa na ugonjwa huo kufikia Jumamosi.

Vilevile, amefichua kuwa wagonjwa wengine 17 zaidi wamepona na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Hii ina maana kuwa kufikia Jumamosi jumla ya watu 301 wamepata afueni.

“Inasikitisha kuwa asilimia 30 ya vifo vilivyothibitishwa, vilitokea nyumbani. Hii inaashiria kuwa ugonjwa huu unasambaa kwa kasi mno katika jamii,” Rais Kenyatta amesema.

“Natuma salamu zangu za pole kwa jamaa na marafiki za waliofariki,” akaongeza.

Rais Kenyatta ameelezea hofu kuhusu ongezeko la idadi ya visa vya maambukizi vinavyotoka nje ya mipaka ya taifa hili.

“Jumla ya visa 43, kati ya visa 166 vilivyoripotiwa kote nchini wiki hii, vilitoka maeneo ya mipaka yetu na mataifa ya Tanzania na Somalia. Na madereva 78 ambao walikatazwa kuingia nchini kutoka Tanzania baada ya wao kupatikana na virusi hivyo,” ameeleza.

Kulingana na Rais Kenyatta visa hivyo 43 vya maeneo ya mpakani vilithibitishwa katika miji kama vile, Wajir (visa 14), Isebania (10), Namanga (16), Lungalunga (2) na Loitoktok (1).

Kiongozi amesema madereva watakaokuwa na cheti cha vipimo vya Covid-19 na watakaokuwa salama kiafya pekee ndio wataruhusiwa kuingia nchini.

“Kwa madereva wanaoingia hapa nchini, lazima wakaguliwe na kupimwa. Watakaoruhusiwa kuingia wawe salama dhidi ya ugonjwa huu,” Rais Kenyatta ameagiza.

Serikali ikiendelea kuimarisha jitihada za kuzuia usambaaji wa virusi vya corona kupitia maeneo ya mipakani, amri ya watu kuingia na kutoingia nchini pia imetolewa.

“Mizigo pekee ndiyo itaruhusiwa kuingia,” akasema Rais, mipaka ya Tanzania na Somalia ikilengwa zaidi kutokana na ongezeko la visa vya raia wa kigeni wanaoingia nchini kupitia njia za mkato.

Mipaka ya Namanga inayounganisha Kenya na nchi jirani ya Tanzania pamoja na ule wa Somalia na Kenya, imekuwa ikimulikwa kwa muda wa siku kadhaa zilizopita.