COVID-19: Kenya sasa ina visa 887
Na CHARLES WASONGA
KWA mara ya kwanza tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kigunduliwe nchini Machi 13, 2020, watu 57 wamepatikana na ugonjwa huo ndani ya muda wa saa 24.
Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Jumapili jioni, serikali imesema hiyo inafikisha 887 idadi jumla ya watu walioambukizwa Covid-19 kote nchini kufikia Jumapili, Mei 17, 2020.
Visa hivyo vipya viligunduliwa baada ya sampuli 2,198 kufanyiwa uchunguzi, idadi kubwa zaidi ya sampuli kuwahi kupimwa ndani ya saa 24.
Miongoni mwa wagonjwa hao 59 ni kwamba 34 ni wanaume huku 23 wakiwa wanawake.
Mgonjwa mwenye umri mdogo zaidi, miongoni mwao ni wa umri wa miaka miwili huku mkubwa zaidi akiwa na umri wa miaka 61.
“Kwa ujumla sampuli 43,712 zimepimwa tangu Machi 13 hadi sasa, kote nchini,” ikasema taarifa iliyotiwa saini na Msemaji wa Serikali Cyrus Oguna.
Kwa mara nyingine Waziri wa Afya Mutahi Kagwe au manaibu wake Dkt Rashid Aman na Dkt Mercy Mwangangi hawakuwahutubia wanahabari katika makao makuu ya wizara hiyo kufafanua hali ya janga hilo nchini, kama ambavyo imekuwa ada.
Hii ni siku moja baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuongeza muda wa kafyu nyakati za usiku kote nchini kwa siku 21 zaidi sawa na amri ya kutoingia na kutoondoka kaunti za Nairobi, Mombasa, Kilifi, Kwale na Mandera.
Vilevile, Rais Kenyatta alifunga mipaka ya Kenya na mataifa ya Somalia na Tanzania kama hatua ya kuzuia visa vya maambukizi ya corona kutoka mataifa hayo.
Hata hivyo, aliruhusu uchukuzi wa bidhaa ila akaamuru kuwa sharti madereva na mataniboi wabainike kutokuwa na virusi hivyo kwanza kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini Kenya.