• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:55 PM
KURA: Gozi la EPL litaanza Juni 12 lakini hili linategemea angalau klabu 14 ziseme “ndio”

KURA: Gozi la EPL litaanza Juni 12 lakini hili linategemea angalau klabu 14 ziseme “ndio”

Na CHRIS ADUNGO

VIKOSI vya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) vinatarajiwa kuwapa wachezaji wao idhini ya kuanza mazoezi ya pamoja katika makundi wiki hii.

Ingawa hivyo, zipo hisia tofauti miongoni mwa washiriki wa kipute hicho ambao wanataka tarehe ya Juni 12, 2020 ambayo soka ya Uingereza inatarajiwa kurejelewa kusogezwa mbele zaidi hadi janga la corona litakapodhibitiwa kwa asilimia kubwa kote duniani.

Maamuzi muhimu kuhusu jinsi ambavyo kampeni za EPL zitarejelewa chini ya mwongozo wa masharti makali ya afya yanatarajiwa kutolewa asubuhi ya Mei 18 katika mkutano utakaohusisha wasimamizi wa klabu zote 20 za ligi hiyo.

Iwapo pendekezo la kuanza upya kwa soka ya EPL mnamo Juni 12 litaidhinishwa, basi wachezaji wataruhusiwa kushiriki mazoezi ya pamoja wakiwa katika makundi ya watu watano kuanzia Jumanne ya Mei 19, 2020.

Ingawa hivyo, watatakiwa kudumisha umbali wa hadi mita moja na nusu kati yao na kuzingatia kanuni zote zilizopo katika juhudi za kukabiliana gonjwa la Covid-19.

Kati ya masharti hayo ni kila mchezaji kufika ugani akijiendesha kwa gari lake huku akiwa tayari amevalia jezi za kujifanyia mazoezi.

Takriban klabu 14 kati ya 20 za EPL zinatakiwa kupiga kura ya ‘NDIO’; yaani kuafikiana kwamba mwongozo wa kanuni mpya za afya zitakazotolewa na maafisa wa afya kwa ushirikiano na serikali na vinara wa soka ya Uingereza utakuwa salama kwa washikdau wa mchezo huo.

Licha ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson kufungua milango kwa soka ya Uingereza kurejelewa, wapo wadau wanaodidimiza tumaini la kuanza upya kwa kivumbi cha EPL.

Kufikia sasa, klabu za Watford, Brighton na Aston Villa zimetishia kujiondoa kwenye kampeni zilizosalia msimu huu baada ya kupinga pendekezo la vikosi kutokubaliwa kuchezea katika viwanja vyao vya nyumbani. Isitoshe, wamekariri kwamba watakosa huduma za baadhi ya masogora wao mahiri zaidi ambao wameathiriwa na janga la corona kwa njia moja au nyingine, kiasi cha kutowezeshwa kurejea kambini kwa michuano iliyosalia.

“Ipo hofu miongoni mwa wachezaji. Sioni kiini cha pupa katika kurejelea kipute cha EPL wakati ambapo wadau muhimu, ambao ni wachezaji, wametangaza msimamo. Kwa wengine, huu ndio wakati wanapohitajiwa zaidi na wapendwa wao” akasema Mwenyekiti wa Watford, Scott Duxbury katika kauli iliyoungwa mkono na kocha Dean Smith wa Villa na Afisa Mkuu Mtendaji wa Brighton, Paul Barber.

Awali, beki Danny Rose wa Tottenham Hotspur alikashifu na kupinga vikali mipango ya kurejesha kivumbi cha EPL kabla ya virusi vya homa kali ya corona kudhibitiwa vilivyo kote duniani.

“Soka haistahili hata kuzungumziwa kwa sasa hadi wakati ambapo idadi ya visa vya maambukizi itashuka kabisa. Maisha ya watu yamo hatarini,” akatanguliza Rose, 29.

Mnamo Mei 12, Chama cha Wachezaji wa Soka Duniani (PFA) kilifichua kwamba kilikuwa kimepokea malalamishi mengi kutoka kwa wanasoka ambao wana “hoja nzito” zinazopania kupinga hatua ya kurejelewa kwa kampeni za msimu huu katika mataifa mbalimbali.

Kwa upande wake, Sadiq Khan ambaye ni Meya wa London, Uingereza alisema kwamba ni “mapema sana” kuanza kujadili uwezekano wa kusakata soka katika jiji kuu la Uingereza wakati ambapo maelfu ya watu wamepoteza maisha huku idadi kubwa ya wakazi wakiugua.

“Mbona tuwe wabinafsi kiasi hicho, tusifikirie familia zilizoathiriwa na maisha ya wale ambao tutakuwa tukiwaweka katika hatari zaidi ya kuambukizwa “gonjwa hili la ajabu” kwa sababu ya tamaa?” akauliza Khan.

Kauli ya Rose ambaye kwa sasa anachezea Newcastle United kwa mkopo kutoka Tottenham, iliwahi kuungwa mkono na nahodha wa Watford, Troy Deeney na fowadi Sergio Aguero wa Manchester City aliyesema wachezaji ‘wanaogopa sana’ kurejea uwanjani kusakata mpira wakati huu.

You can share this post!

Klabu yatumia madoli kama ‘Samantha’ yawe...

AFYA: Panyako na wenzake waahirisha mgomo kwa siku 21

adminleo