• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Nahodha wa Watford asema harejei kambini kabla corona kuisha

Nahodha wa Watford asema harejei kambini kabla corona kuisha

CHRIS ADUNGO na MASHIRIKA

NAHODHA wa Watford, Troy Deeney, amesema hatarejea katika kambi yao uwanjani Vicarage Road kwa mazoezi yanayofanywa sasa na wanasoka wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa minajili ya kampeni zilizosalia msimu huu wa 2019-20.

Nyota huyo mzawa wa Uingereza ameshikilia kwamba anahofia uwezekano mkubwa wa kuambukiza familia yake virusi vya corona iwapo atakuwa sehemu ya watakaorudi kambini mwa mazoezi.

“Ipo hofu miongoni mwa wachezaji, mimi nikiwwamo. Sijaona kabisa sababu ya pupa katika kurejelea kipute cha EPL wakati ambapo baadhi yetu tunahitajiwa zaidi na wapendwa wetu,” akasema Deeney katika kauli ambayo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa kikosi cha Watford, Scott Duxbury.

Kwa mujibu wa magazeti mengi ya Uingereza, Deeney ana mtoto aliye na matatizo ya kupumua na huenda akawa katika “hatari zaidi” ya kuambukizwa ugonjwa wa corona ambao umewalemea zaidi wachezaji wenye asili ya Kiafrika na Asia nchini Uingereza.

Deeney, Sergio Aguero wa Manchester City na Danny Rose wa Tottenham Hotspur ni miongoni mwa wachezaji ambao wamejitokeza kukashifu hatua ya kurejelewa kwa kipute cha EPL wakati ambapo janga la corona bado halijadhibitiwa vilivyo duniani.

“Tunatarajiwa na kikosi chetu kurejea kambini wiki hii. Nimewaambia kwamba sitakuwa sehemu ya wale watakaorudi Vicarage Road,” akasema Deeney, 31.

Licha ya wachezaji wa klabu za EPL kuidhinishwa kurudi mazoezini wakiwa katika makundi ya hadi wanasoka watano kwa pamoja, Watford hawajaanza kujifua kwa minajili ya mechi tisa zaidi ambazo zimesalia muhula huu.

Katika mahojiano yake na gazeti la The Times, Uingereza, kocha Nigel Pearson wa Watford alisema kwamba hatawalazimisha wachezaji wake kurejea kambini kwa mazoezi na klabu imeshikilia kwamba maamuzi ya kurudi ni hiari ya mtu.

Kwa upande wake, Deeney ameshikilia kwamba, “Inahitaji mtu mmoja pekee kupata virusi vya corona na kikosi kizima kuathirika. Nisingependa kabisa kuleta ugonjwa huu nyumbani kwangu.”

“Mtoto wangu wa kiume ana umri wa miezi mitano pekee na ana matatizo ya kupumua. Sitaki kurudi nyumbani na corona na kuhatarisha maisha yake zaidi,” akasema Deeney.

Kwa mujibu wa idara inayohusika na takwimu za kitaifa nchini Uingereza, ‘watu weusi’ wapo katika hatari ya asilimia kubwa zaidi kuaga dunia kutokana na corona nchini Uingereza na Wales kuliko wale weupe.

Mnamo Mei 13, 2020, Deeney alikuwa katika mkutano ulioleta pamoja maafisa wa afya, vinara wa EPL na manahodha wa kipute hicho. Mshambuliaji huyo aliuliza baadhi ya maswali yaliyowashinda walioshiriki kikao hicho kujibu.

“Je, zaidi ya kupima tu corona, wanasoka watakuwa pia wakipimwa ili kubaini iwapo wana matatizo ya ziada kama vile ya moyo?” akatanguliza.

“Mmesema mtu hastahili kwenda kinyozi kunyolewa hadi katikati ya Julai kwa sababu ya corona. Je, nikiwa nawania mpira wa kona kwa pamoja na wanasoka wengine 19 ndani ya kijisanduku cha timu pinzani, nini kitanizuia kuambukizwa?” akauliza.

You can share this post!

Kagwe awapongeza Wakenya kwa kutilia maanani taratibu na...

Seneta Ledama ole Kina aitwa mahakamani ajibu shtaka la...

adminleo