Habari

Ichung'wah asema haogopi kupokonywa wadhifa wa mwenyekiti kamati ya bajeti

May 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Kikuyu Kimani Ichung’wah amesema haogopi kupokonywa wadhifa wake wa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Bungeni akisema ataendelea kukosoa mabaya yanayoendelea serikalini na hata katika chama cha Jubilee.

Akiongea wakati wa mahojiano katika runinga ya Citizen Jumanne usiku Bw Ichung’wa hata hivyo alishikilia kuwa ataendelea kuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto katika jitihada zao za kutimiza ajenda zao za maendeleo.

“Nitaendelea kumuunga mkono kiongozi wa chama chetu pamoja na naibu wake katika utekelezaji wa Ajenda Nne za Maendeleo. Na hiyo ndio nimekuwa nikifanya kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na nitaendelea nayo hata nikipokonywa wadhifa huo,” Bw Ichung’wa akasema.

“Ninapounga mkono Rais Kenyatta, namtarajia kuheshimu demokrasia kwa kuniruhusu kutoa kauli tofauti kuhusiana na masuala mengine,” akaongeza.

Bw Ichungwa alisema kumuungano mkono Rais Kenyatta hakumaanishi kuwa sharti akubaliane naye kwa kile kitu.

Mbunge huyo wa Kikuyu na ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto alisema yuko radhi kuendelea kuwatumikia wakazi wa eneobunge hilo ikiwa kufanya hivyo kutamruhusu kushikilia misimamo huria ya kisiasa bila kudhibitiwa.

Bw Ichung’wah alisema maadui wa Rais Kenyatta ni wale ambao hawamuambii ukweli; wale ambao wanataka kuendesha chama cha Jubilee kama mali yao binafsi.

“Ningependa kuwaeleza kuwa chama cha Jubilee ni asasi ya umma inayofadhiliwa na pesa za umma na ambayo inaongozwa na Katiba pamoja na sheria nyinginezo. Kwa hivyo, maamuzi mazito ya chama ni muhimu yafanywe kulingana na masharti yaliyowekwa kwenye Katiba hiyo,” akaeleza huku akikosoa mpango uliopo unaolenga kuondolewa kwa naibu spika wa seneti Profesa Kithure Kindiki.

Hata hivyo, Bw Ichung’wah alisema kuwa mgogoro uliopo ndani ya Jubilee unaweza kusuluhishwa ikiwa masuala ya chama yataendeshwa kwa taratibu na sheria zilizopo.

“Ikiwa tunataka kubadili uongozi bungeni, sharti tufuate taratibu zilizowekwa,” Bw Ichung’wah akaeleza.

Aidha, alihoji mbinu iliyotumiwa kuwaondoa maseneta Kipchumba Murkomen na Susan Kihika kutoka nyadhifa za Kiongozi wa Wengi na Kiranja wa Wengi, mtawalia.